Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel amekutana na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ireland wenye nia
ya kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini na kuwataka kuangalia
zaidi mnyororo wa thamani wa namna ya kuyaongezea thamani maziwa ili
kupanua zaidi soko la maziwa kutoka Tanzania kwenda nchi za nje.
Akizungumza
na wawekezaji hao leo (Jumatatu 30.09.2019) kutoka shirika la
Sustainable Food Systems Ireland (SFSI) ofisini kwake katika Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma, Prof. Gabriel amesema maziwa
yatakapoongezewa thamani yataiwezesha Tanzania kuingia zaidi katika
masoko ya nje ya nchi yakiwemo ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya
Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
“Waangalie
pia zaidi mnyororo wa thamani namna ya kuyaongezea maziwa thamani ili
tuingie zaidi katika solo la Afrika Mashariki, SADC na nje ya SADC.
Lengo kubwa la wizara kwa wadau kama hawa wakija kutuona inakuwa faraja
kwa kuwa inagusa maisha ya mfugaji wa kawaida, pale ambapo maziwa
yatachakatwa na kuongezewa thamani soko litakuwepo tungependa wafugaji
wazalishe maziwa ambayo wataweza kuuza.” Amesema Prof. Gabriel
Ameongeza
kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha
inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili soko la maziwa
liendelee kuwepo kwa kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita
Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo yanapaswa kuongezewa thamani ili kukuza
zaidi soko la maziwa ndani na nje ya nchi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa shirika la SFSI ambalo lipo chini ya Wizara
ya Kilimo, Chakula na Bahari ya Jamhuri ya Ireland Bw. David Butler,
amesema shirika hilo ilimekuwa likifanya kazi katika nchini mbalimbali,
ambapo limekuwa likifanya vizuri katika sekta ya nyama na maziwa kwa
zaidi ya miaka 40 na kuendesha programu mbalimbali za kilimo na mifugo
ili kuyaongezea thamani mazao.
Bw.
Butler ameambatana na Dkt. Seamus Crosse kutoka Shirika la Greenfield
International la Jamhuri ya Ireland, ambapo wawekezaji hao watakutana na
wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo
chini ya wizara hiyo ili kuangalia namna ya bora ya uwekezaji katika
tasnia ya maziwa nchini.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano serikalini
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Post A Comment: