Friday, 6 September 2019

WAKULIMA ,WAFANYAKAZI WA MKONGE WALIA KWA DC KOROGWE

 Baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Mkonge Hale kilichopo chimi ya Kampuni ya Katani Ltd wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Kasongwa (hayupo pichani) alipofika kiwandani hapo kuzungumza nao. (Picha na Yusuph Mussa).
Attachments area
Mkonge huu wa mmoja wa wakulima wa Shamba la Mkonge Hale wilayani Korogwe ambao umeharibika, unadaiwa kuvunwa Mei 3, 2019 kisha kutelekezwa ukiwa shambani.

Na Yusuph Mussa, Korogwe


BAADHI ya wafanyakazi na wakulima wa Shamba la Mkonge Hale lililopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamelalamika kuwa hawaridhiki na mwenendo wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Mkonge Hale (AMCOS).


Walitoa dukuduku lao juzi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Kasongwa alipotembelea Kiwanda cha Mkonge Hale kilichopo chini ya Kampuni ya Katani Ltd ili kusikiliza changamoto za wafanyakazi ikiwa ni muendelezo wa kutembelea viwanda vya mkonge vya Magoma, Mwelya, Ngombezi, Magunga na Hale.


"Mkuu wa Wilaya mimi nilipewa kazi ya usimamizi na AMCOS ya Hale ya kusimamia wakataji na kuwalipa. Na kazi hiyo ya malipo nilikuwa naifanya kila jumamosi.  Lakini nilisimamishwa kazi baada ya kuambiwa nimepoteza mkonge wa wakulima. Nataka kusema mbele yako, mkonge ulikuwepo na meta zilizokatwa zilikuwa sawa, lakini kuna watu ili kunihujumu, walichukua baadhi ya mkonge huo na kwenda kuutupa ili meta zangu ziwe pungufu.


"Bado kuna mkonge mwingine umebaki eneo hilo, kwani una muda mrefu ulikuwa umekatwa (tangu Mei 3, 2019), lakini ulishindwa kusombwa kwa wakati ili uweze kufikishwa kiwandani. Hofu yao ni kuwa mkonge huo ungeletwa kiwandani wakati muda umepita, mkonge wake ungekuwa wa daraja la chini sana... Mkuu wa Wilaya, nipo tayari kuweka mafuta kwenye gari lako ili ukaone mkonge huo uliotelekezwa shamba" alisema Omar Chuma.


Mkulima Emmanuel Cossam alisema, mkonge wake haujakatwa kwa muda mrefu huku yeye akiwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kumuuguza baba yake. Hivyo kumuomba Mkuu wa Wilays aweze kumsaidia ili mkonge wake ukatwe.


"Mimi nimekuwa nalia na uongozi wa AMCOS wanisaidie namna ya kukata mkonge ili nimuuguze baba yangu mzazi ambaye anaumwa ugonjwa wa tezidume, lakini sasa ni muda mrefu na kilio changu hakijasikilizwa, hivyo Mkuu wa Wilaya, naomba unisaidie kwa hilo" alisema Cossam.


Kasongwa alitaka kujua uongozi kama unayajua malalamiko hayo, huku akiagiza uongozi wa AMCOS, pamoja na kuwa wanakata mkonge kwa zamu, lakini mkulima anaeuguliwa na baba yake apewe kipaumbele ili aweze kumuuguza mzazi wake.


"Korogwe ndiyo wilaya inayoongoza kwa kilimo cha mkonge Tanzania nzima. Naomba sifa hizo ziendane na hali halisi, sio watu tunasifiwa nchi nzima, halafu wakulima na wafanyakazi wake wa mkonge choka mbaya! nataka kampuni ya Katani Ltd na AMCOS muhakikishe mnawalipa kwa wakati wakulima na wafanyakazi wa mkonge" alisema Kasongwa.


Hata hivyo, Kasongwa aliipongeza Kampuni ya Katani Ltd, kwani katika viwanda vitano vya kusindika mkonge vya Hale, Mwelya, Ngombezi, Magunga na Magoma, Kiwanda cha Hale, wafanyakazi wanadai mshahara wa nusu mwezi wa Agosti, mwaka huu, tena ni kwa sababu Katani Ltd hawajalipwa sh. milioni 18 na AMCOS.


"Wafanyakazi wa Katani Ltd, niseme ninyi hapa mna maisha mazuri tofauti na wenzenu. Huko kote nilikopita, ninyi peke yenu ndiyo mnadai fedha kidogo tangu utaratibu mpya umeanza wa kuwa chini ya AMCOS... tena mnadai nusu mwezi. Nina hakika baada ya Katani Ltd kulipwa hizo fedha, nao watawalipa mshahara wenu" alisema Kasongwa.


Meneja wa Kiwanda cha Mkonge Hale Nassoro Mpate alisema wanaidai AMCOS sh. milioni 18, huku Mwenyekiti wa AMCOS Hale Abdallah Kamili akikiri deni hilo, na kudai wangelipa fedha hizo kwa Katani Ltd wiki hii ili nao wawalipe wafanyakazi.


Kamili aliahidi kushughulikia malalamiko hayo ya wakulima na wafanyakazi, huku akiahidi kumpa kipaumbele Cossam ili avuniwe mapema mkonge wake ili aweze kumuuguza mzazi wake, na huku akiahidi kufuatilia suala la mkonge kutupwa na mwingine kuachwa shamba wakati ulishakatwa.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Sept. 5, Kamili alisema hana uhakika na tuhuma zilizotolewa kuhusu mkonge kutupwa porini na mwingine kuachwa shambani, lakini kesho Jumamosi (Sept. 7), Kamati ya Nidhamu ya AMCOS Hale itakaa na wahusika ili kuweza kujua ukweli wa jambo hilo.


"Mwandishi, unaposema una ushahidi wa picha ya mkonge uliotupwa ama kuachwa shamba, mimi hilo siwezi kuthibitisha, unajuaje kama huo mkonge ni wa sehemu hiyo. Ili kupata ukweli wa hilo, Kamati ya Nidhamu ilikuwa ikae leo (jana), lakini kutokana na vikao vingi hapo Korogwe, kikao hicho kitafanyika Jumamosi" alisema Kamili.


MWISHO.

No comments:

Post a comment