Sunday, 8 September 2019

Wakazi wa Olasiti wametakiwa kurasimisha maeneo yao.Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Afisa Tarafa Elerai Titho Cholobi amewataka Wakazi wa kata ya  Olasiti kurasimisha maeneo yao kwa kuyapima na kuyakatia hati ili kuepuka migogoro ya ardhi ambayo imekua ikiathiri maendeleo na kusababisha migongano isiyo na tija.

Akizungumza katika mkutano wa kurasimisha ardhi uliofanyika katika Mtaa wa Olasiti kati kata ya olasiti wilaya ya Arusha,Cholobi amewataka wakazi hao kuyapima maeneo hayo na kuyapatia hati ili yaweze kuwa na ulinzi wa kisheria hivyo kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Cholobi amesema kuwa kwa sasa serikali imetoa fursa kwa wananchi wake kupimiwa ardhi kwa gharama nafuu ili waweze kurasimisha maeneo yao.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Upimaji ardhi ya Al.Land Planning Tanzania ltd  Levisy Adriano  amesema kuwa fursa hiyo itawawezesha wananchi kuweka mpango wa pamoja wa kupima maeneo yao kwa gharama nafuu  hivyo amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Diwani kata ya Olasiti  Alex Marti amesema kuwa zoezi la urasimishaji limekuja katika wakati muafaka na kuhakikisha  wananchi hao wanapimiwa maeneo yao na kupatiwa hati ili kuweza kutumia ardhi kama aseti ya kuweza kukopesheka na kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Mtaa  wa Olasiti kati ,Bruno Mbole ameipongeza serikali na kampuni hiyo ya upimaji kwa kuweza kuwafikia wananchi katika Mtaa yao na kuwapimia ardhi zao.

No comments:

Post a comment