Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd Juma Shamte. (Picha na Yusuph Mussa).

Na Yusuph Mussa, Tanga


KAMPUNI ya Katani Ltd imepokea kwa matumaini makubwa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa aliyofanya kwenye viwanda saba vya kusindika mkonge, na hasa alipoagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuchunguza vitendo vya wizi na ubadhirifu.


Ni kutokana na ziara hiyo aliyofanya Septemba 2, mwaka huu, kwenye viwanda hivyo vilivyopo kwenye mashamba ya Mwelya, Magoma, Magunga, Hale na Ngombezi, kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima na wafanyakazi wa Katani Ltd kuwa baadhi ya wakulima kudai mkonge wao unakatwa na kuuzwa, lakini fedha wanapewa watu wengine.


Huku wafanyakazi waliojiriwa na Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Mkonge (AMCOS) kudai wanafukuzwa kwa tuhuma ambazo ni za kutunga, na wafanyakazi waajiriwa wa Katani Ltd kudai wanadai mishahara yao ya malimbikizo kutoka kwa kampuni hiyo.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Septemba 11 akiwa ofisini kwake jijini Tanga, Shamte alisema wana imani maagizo yake yatafanyiwa kazi, na baada ya TAKUKURU kumaliza kazi kwenye baadhi ya viwanda hivyo ukweli utajulikana.


"Tumepokea ziara ya Mkuu wa Wilaya ambayo tumefurahi kuja kwake na kujionea mwenyewe ufanisi wa chama (AMCOS) na kuagiza TAKUKURU kwenda kuchunguza. Mfano vyama kutolipa madeni yao yote kwa kampuni, wakulima na watoa huduma wengine, na kuangalia mapungufu mengine ambayo ni ya wakulima na wafanyakazi.


"Tunatarajia uchunguzi huu utaweza kuthibitisha madai ya kampuni ambayo yakilipwa yatakwenda  kulipa sehemu ya madai ya wafanyakazi kama yalivyopangwa tangu Januari, mwaka huu. Lakini pia tunashukuru ziara ya DC, pia imeibua changamoto mbalimbali, na kama zitafanyiwa kazi, itaongeza ufanisi kwa viwanda vya kampuni na kutoa haki kwa wafanyakazi, ama kampuni na wafanyakazi wake" alisema Shamte.


Kwenye ziara hiyo Mkuu wa Wilaya Kasongwa alipokea malalamiko ya baadhi ya wakulima kwenye Kiwanda cha Mkonge Magunga, kuwa mkonge wao unavunwa na kuuzwa, lakini fedha wanaingiziwa watu wengine kwenye akaunti zao za benki. Lakini pia kulikuwa na harufu ya ubadhirifu wa fedha kwenye kiwanda hicho, kwani Meneja wa Kiwanda cha Mkonge Magunga Abdulrahman Zayumba alisema anaidai AMCOS ya Shamba la Mkonge Magunga.


Lakini Mwenyekiti wa AMCOS hiyo Eliamini Mrutu anasema Kampuni ya Katani Ltd haina deni lolote kwao, huku akikanusha wakulima kuvuniwa mkonge wao huku fedha wakipewa watu wengine. 


Wakati kwenye Kiwanda cha Mkonge Hale, baadhi ya wafanyakazi walioajiriwa na AMCOS walisema wamefukuzwa kazi kwa kueleza wamepoteza mkonge wa wakulima, wakati mkonge huo umevunwa, lakini umeshindwa kufikishwa kiwandani kwa wakati, hivyo kuachwa shambani na kuharibika. Lakini Mwenyekiti wa AMCOS ya shamba hilo Abdallah Kamili, alikanusha jambo hilo na kusema atafanya uchunguzi.


Lakini kwenye Kiwanda cha Mkonge Ngombezi, wajumbe wawili wa AMCOS, Agosti 25, mwaka huu, walijiuzulu kwa madai hawaridhiki na  utendaji wa AMCOS hiyo, huku wakimtupia lawama Mwenyekiti wa AMCOS hiyo Aggrey Nnyari kuwa anafanyakazi nyingi za AMCOS hiyo bila kuwashirikisha wajumbe. Hata hivyo Nnyari alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alikanusha kufanya maamuzi bila kuwashiriki wajumbe.


MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: