Monday, 9 September 2019

BREAKING NEWS : Maombi ya Tundu Lissu yakataliwa na Mahakama


Mahakama Kuu imekataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.

Imesema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Akisoma uamuzi huo wa mahakama leo Jaji Sirillius Matupa amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Ikumbukwe Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

No comments:

Post a Comment