Kulia ni Simon Mdoe, Mtafiti Mwandamizi wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ( TAEC) akitoa elimu kwa wageni waliotembelea Banda la  TAEC kwenye maonesho ya kilimo ya nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya TASO vilivyoko Njiro Jijini Arusha
Peter Ngamilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ( TAEC) akitoa elimu kwa wageni waliotembelea Banda la  TAEC kwenye maonesho ya kilimo ya nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya TASO vilivyoko Njiro Jijini Arusha


Na.Vero Ignatus,Arusha

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeeleza kuwa utafiti wa mbegu ya mpunga kwa kutumia teknolojia ya nyuklia ya kununurisha vinasaba (viasili) umefanikiwa kupata matokeo chanya ya kupata mbegu bora ya Super BC yenye kuleta mavuno mengi zaidi visiwani Zanzibar.

Akizungumza jana na Mwandishi wa habari hizi kwenye viwanja vya maonyesho ya nane nane kanda ya kaskazini yaliyopo Eneo la Themi jijini Arusha yenye ujumbe wa mchango wa teknoljia ya nyuklia kwenye kilimo, mifugo kwa ukuaji wa uchumi wa Nchi, Mtafiti mwandamizi wa teknolojia ya Nyuklia, Simon Mdoe alisema utafiti huo ulioanza 2009 umefanikisha matokeo chanya mara saba zaidi kwa mavuno ya mbegu ya mpunga ya Super BC huko visiwani Zanzibar ikilinganishwa na awali.

Mdoe alisema utafiti wa mbegu hiyo uliofanywa na Kituo cha utafiti wa kilimo cha Zanzibar, (ZARI) na pamoja na chuo cha kilimo cha Sokoine (SUA), unaratibiwa TAEC kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki duniani (IAEA) ambapo walinunurisha (kupitisha mionzi kitaalamu kwenye mbegu) ambayo ilibadilisha viasili (vinasaba) na kuwa bora zaidi kuweza kuzalisha mara saba ya mazao yaliyokuwa yakizalishwa awali.

Katika utafiti wetu tulichukua mbegu za mmea wa mpunga na kupitisha miale ya nyuklia kwa hatua sita, huku kila hatua moja tukihamishia mbegu shambani na kupata matokeo tofauti, mara ya mwisho tulipata matokeo mazuri zaidi kuliko hatua nyingine tano na kugundua kuwa na mavuno yamefikia mara saba ya kawaida ya mbegu hizo…kama mkulima anavuna magunia 12 kama ambavyo imezoeleka kwa mbegu za zamani na alipotumia mbegu za super BC alipata gunia 70 za mpunga.alisema Mdoe.

Alisema baada ya matokeo ya utafiti ulishirikishwaji ulifanyika kwa mashirika ambapo mbegu hizo za Super BC zilitawanya kwenye maduka ya mbegu visiwani Zanzibar na kuwapelekea wakulima ambao walipata matokeo  hayohayo mazuri mara saba zaidi tofauti na awali kabla ya utafiti. Asilimia takriban 80 ya wakulima Zanzibar wanapendelea kutumia mbegu hii

Mdoe alisema pia matokeo mengine ya utafiti na kuboreshwa kwa mbegu kupitia mionzi ya nyuklia yamebaini kuongezekana kwa ladha ya mchele uliotokana na mpunga wa Super Bc, pamoja na harufu nzuri kwa walaji.

“Alisema pia matokeo ya tafiti yameonyesha mbegu hiyo kutoshambuliwa na wadudu wakati wa kuota na ukuaji wake”alisema Mdoe. Utafiti bado unaendelea ili kupata mbegu zingine bora zaidi zikiwemo za mahindi na shayiri

Mtafiti hiyo alisema TAEC kwa kushirikiana na Chuo cha kilimo cha Sokoine (SUA) wanaendelea na utafiti ili kununurisha mbegu nyingine za mpunga, zaidi ya Super Bc kwa kuzingatia hali ya hewa na maeneo tofauti tofauti ya Nchi na aina ya udongo ili kupata ili kupata tija itokanayo na mavuno mengi kwa ustawi wa Uchumi wa Nchi.

Mdoe alisema utafiti wa kununurisha mbegu hizo  unafanyika pia kwenye kituo cha utafiti cha Ilonga Mkoani Morogoro na katika kituo cha Mati kilichopo eneo la Uyole Jijini Mbeya.

Aidha alisema kuna Tafiti nyingine kama hizo za mbegu za Mahindi na shairi zinazofanyika katika Kituo cha utafiti wa mbegu za Kilimo cha SELIAN, Arusha ambazo ununurishaji umeshafanyika na tayari mbegu hizo ziko kwenye hatua za mpando wa awali ambapo hatua nyenye ubora wa juu utakapofiki tamati, zitasambazwa kupitia njia zilizofanyika Zanzibar kwa wakulima ili kuongeza mavuno na kukuza uchumi wa wakulima na Taifa kwa pamoja.

Alisema pia TAEC na taasisi ya mboga mboga, maua na matunda ya (TAHA) kwa pamoja wako kwenye upembuzi yakinifu ili kuona namna ya kununurisha mboga mboga, matunda na maua ili kuhifadhika kwa muda mrefu na unaofaa pindi bidhaa inapokuwa sokoni kwa muda ili isiharibike kwa urahisi kwani uzoefu unaonyesha asilimia 40 ya matunda na mbogamboga huharibika kwa kuoza kutokana na kukosa au kutokutumia teknolojia kama hiyo ya mionzi.

Alisema tafiti nyingine zinafanyika kwenye mbegu za wanyama kama Ng’ombe kwa njia ya uhimilishaji inayofanywa na Taasisi ya mifugo ya uhimilishaji ya NAIC iliyopo USA Liver ili kupata mifugo bora inayokidhi viwango vya ndani na nje kwa nyama bora.

Naye mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wanTAEC, Peter Ngamilo alisema TAEC ina matarajio ya kuwa na mtambo wa kuzalisha vyanzo vya mionzi (Linear Acceletor) vinavyotumika kwenye matibabu, viwanda, kilimo na utafiti (Radioisotopes)

Alisema Pia TAEC  ina matarajio ya kuanzisha mradi wenye kutumia teknolojia ya nyuklia katika kufanya tafiti mbalimbali (Nuclear Research Reactor) Zenye manufaa kwa Nchi.

Mtambo huo utaiwezesha Tanzania kuwa na viwanda vya madawa ya tiba ya saratani pamoja na kutumika kama nyenzo ya kufundishia katika taasisi za elimu ya juu na utafiti.

Tume ya Nguvu ya Atomiki (Tanzania Atomic Energy Commission) ilianzishwa kwa  sheria ya Bunge no 7 ya Mwaka 2003, awali ilikuwa ikijulikana kama Tume ya taifa ya mionzi iliyoanzisha kwa sheria ya bunge no 5 Mwaka 1983. TAEC ina majukumu ya kuthibiti na kusimamia matumizi salama ya mionzi  Nchini, kuhamasisha na kuendeleza matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia  na kufanya utafiti na kutoa ushauri na taarifa mbali mbali juu ya Sayansi na Teknolojia ya nyuklia.

MWISHO
Share To:

Vukatz Blog

Post A Comment: