Afisa Tarafa wa Elerai Titho Cholobi ameagiza wezi walioba mboga mboga katika bustani ambazo ni mradi unaofadhiliwa na Tasaf katika  eneo la shule ya msingi Lemara wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwani wamehujumu fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kaya masikini ziweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea miradi inayotekelezwa na serikali ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya msingi Lemara  ambayo bado haijakamilika pamoja na mradi wa kilimo cha mboga mboga unaofadhiliwa na Tasaf,Afisa huyo ameshangazwa na kitendo hicho ambacho kinawakatisha tama kinamama wanaolima bustani hizo pamoja na wawezeshaji wa mradi huo.

Titho amesema kuwa mradi huo hauna haja ya kuwekewa mlinzi maalumu kwani utaongeza gharama za utekelezaji hivyo polisi jamii wanapaswa kuulinda mradi kwa kushirikiana na wananchi kwani fedha hizo ni za serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Hata hivyo ameuagiza uongozi  wa kata kukutana na kujadili juu ya namna ya kuwashirikisha wadau wa maendeleo katika kumalizia miradi ambayo bado haijakamilika ili iweze kukamilika ikiwemo ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule hiyo ya msingi.
Mwantumu Jumanne ni moja kati ya kinamama wanaolima bustani hizo kati ya wanawake 26 ameeleza kuwa usiku wa kuamkia leo wameamka na kukuta tuta moja la mboga limevunwa kabla ya muda wake majira ya saa tisa usiku jambo ambalo linawaumiza na kuwakatisha tamaa ya kuendelea na mradi huo.
Mtendaji wa kata ya Lemara  Johari Kitara amesema kuwa mradi huo ulianzishwa na Tasaf kwa lengo la kuwakomboa kinamama ili wapate kipato na kujiendeleza hivyo changamoto hiyo itashughulikiwa.
Hadi tunaondoka eneo la tukio tayari watu wawili wamekamatwa na polisi na wamefikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma za wizi wa mboga.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: