Wednesday, 8 May 2019

WAZIRI NDALICHAKO AIPONGEZA UDSM KWA KUTENGA BILIONI MOJA ZA KUENDELEZA UTAFITI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuwawezesha wanataaluma kufanya tafiti zaidi hasa zinazogusa jamii moja kwa moja.

Waziri Ndalichako ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo amesema tafiti ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa kujenga  na kukuza uchumi wa viwanda nchini.

Prof. Ndalichako amesema serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda lengo likiwa kuhakikisha kunakuwa na viwanda ambavyo vinatumika kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zitakazotosheleza jamii ya Kitanzania na kusaidia kuongeza ajira kwa vijana.

Akizungumzia Wiki ya Utafiti Waziri Ndalichako amesema inawapa wadau wa utafiti na ubunifu jukwaa la kufahamu shughuli za utafiti zinazofanyika; sehemu gani kuna mapengo na changamoto; na mikakati gani ya kimipango inahitajika ili kuziba mapengo pamoja na kutatua changamoto zilizobainika.

"kama taifa, tuna wajibu mkubwa na fursa nyingi za kuweza kutumia utafiti, ubunifu na ujasiriamali hususan kupitia sekta ya elimu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda nchini. 

Kufanya hivyo, kutawezesha kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Dira ya Taifa ya 2015, ya kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia uchumi wa kati kupitia viwanda." Amesisitiza Waziri NdalichaKo

No comments:

Post a comment