Thursday, 25 April 2019

WAFANYABIASHARA TUMIENI BANDARI YA TANGA KWANI HUDUMA ZIMEBORESHWA

Katibu Tawala  wa mkoa wa  Kilimanjaro muhandisi Bi.Aisha Amour akizungumza na waandishi Wa habari  katika mkutano  Wa waandishi Wa  habari   ulioandaliwa na mamlaka ya bandari ya Tanga  uliofanyika Leo katika ukumbi Wa mikutano Wa mkuu Wa mkoa Wa Kilimanjaro.

Na Woinde Shizza, Kilimanjaro

Katibu tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Injinia Aisha Amour amewataka wafanyabiashara kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuitumia bandari ya Tanga katika kusafirisha mizigo yao kwani hivi sasa imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwepo kwa mitambo mikubwa na ya kisasa. 

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kilichofanyika mkoani Kilimanjaro kilicholenga kuzungumzia  utendaji kazi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania, bandari ya Tanga. 

Alipongeza mamlaka ya bandari Tanzania chini ya uongozi wa Mhandishi Deusdedit Kakoko Kwa jitihada kubwa za kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma katika kiwango cha hali ya juu katika bandari ya Tanga na kuwa mkakati huo utaifanya bandari hiyo kuwa kimbilio la wafanyabiashara na wawekezaji. 

Alisema kuwa, wafanyabiashara wengi kutoka mikoa hiyo wamekuwa wakitumia kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Mombasa kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo hapo nyuma ambapo hivi sasa bandari hiyo imeboreshwa tofauti na hapo nyuma. 

"jamani tunaombeni Sana wafanyabiashara watumie hii bandari ya Tanga kwani sasa hivi imeboreshwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mitambo mikubwa ya kisasa ambayo ina uwezo mkubwa wa kurahisisha utoaji huduma. "alisema Injinia Aisha. 

Naye Meneja wa bandari ya Tanga, Percival Salama alisema kuwa, bandari hiyo imeweza kuhudumia tani 506,000 Kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 ambapo hadi kufika june mwaka huu watakuwa wamehudumia tani 700,000.

Salama alisema kuwa, bandari hiyo ina jumla ya mitambo 42 Kwa sasa, ambapo kwa mwaka 2018/2019 imeagiza mitambo 20 kati ya hiyo mitambo 16 imeshawasili sawa na asilimia 80 .

Alisema kuwa, hivi sasa changamoto ya swala la mitambo katika bandari hiyo limepatiwa ufumbuzi wa kudumu, hivyo kuwataka wafanyabiashara  wa Arusha na Kilimanjaro sasa kujitokeza Kwa wingi kuitumia bandari hiyo. 

"Kwa kweli bandari ya Tanga ya sasa hivi sio ile tuliyoizoea zamani, sasa hivi bandari imeboreshwa Sana ikiwa ni Jitihada za Mkurugenzi mkuu wa bandari Tanzania, Injinia Deusdedit Kakoko lengo likiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwa wakitumia bandari zingine wanarudi nyumbani kwani sasa kumenoga. "alisema Salama. 


Salama aliongeza kuwa, bandari ya Tanga ndio bandari pekee Afrika yenye uwezo wa kuhudumia nchi 7 kwa  kutumia mpaka mmoja, ambapo nchi hizo ni Malawi, Zambia, DRC Congo, Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya. 

No comments:

Post a comment