KATIBU MKUU wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Susan Mlawi ameagizwa ampangie kazi nyingine Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Bi. Joyce Fisoo na ateue mtu mwingine kushika nafasi hiyo.

Agizo hilo lilitolewa jana jioni (Jumatano, Aprili 24, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akihitimisha kikao chake na wasanii zaidi ya 100 kutoka Shirikisho la Filamu Tanzania kilichofanyika Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

Shirikisho la Filamu Tanzania linajumuisha vyama 11, ambapo 10 vimesajiliwa na kimoja hakijakamilisha usajili. Vyama hivyo ni vya waigizaji, waongozaji, watayarishaji, wahariri, wachekeshaji na wapigapicha. Wengine ni waandishi wa miswada (script writers), watafutaji mandhari, wasambazaji wa filamu, walimu na chama cha wanawake wa tasnia ya filamu ambacho bado kiko kwenye mchakato wa usajili.

Kikao hicho ambacho kilidumu kwa zaidi ya saa saba, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Bibi Juliana Shonza.

“Katibu Mkuu mtafutie eneo jingine la kufanya kazi. Hana tuhuma zaidi ya mahusiano mabaya na wadau wake, ana historia nzuri, lakini tatizo ni mahusiano. Mpeleke idara nyingine na hapa mlete mtu mwingine,” alisema Waziri Mkuu.

“Mama Fisoo wewe uko clean, sina tatizo na utendaji wako lakini ukikaa hapa hutaweza kwenda mbele na wala hawa wote hawatakuja kufanya kazi na wewe. Tunataka hii tasnia iende mbele, tunataka maendeleo kwenye tasnia ya filamu,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania, Profesa Frowin Nyoni ajipange upya na Bodi yake na kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wasanii kama ambavyo imeainishwa kwenye sheria ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo.

“Bodi yako inao wajibu wa kutoa elimu kwa makundi tofauti ya wasanii. Sheria yenu imeainisha kuwa mnapaswa kutoa elimu. Wapeni refresher courses ili waongeze ujuzi na wakienda huko wanatoa uzoefu walionao kwa wanachuo, nao pia wanakuwa wamejifunza,” alisema.

“Nimeangalia makundi ya wasanii na kukuta kuna wachoraji na wachongaji; wasanii wa filamu, wasanii wa maigizo, wabunifu wa mitindo na wote hawa wana Bodi zao. Timizeni majukumu yenu. Bodi pia mna kazi ya kupromote brand kwa kutumia wasanii wetu,” alisema.

Kuhusu utitiri wa tozo ambao umelalamikiwa na wasanii hao, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya kulinda soko la ndani la kazi za wasanii wa Kitanzania tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wazawa wanatumia gharama kubwa kutengeneza kazi zao lakini wanapata shida kuziuza ilhali wageni wanapata faida zaidi kwa kazi kama hizo.

“Wasanii wamesema kuna tozo 11 lakini Mtendaji Mkuu kataja tozo chache tu. Hebu Waziri aitishe kikao baina yenu, Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara, Kamishna wa TRA, Bodi ya Filamu na TCRA, mkutane mara moja na kuziangalia upya hizi tozo ili zipunguzwe kama tulivyofanya kwingine. Lazima tulinde soko la ndani,” alisisitiza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya wasanii juu ya fukuto linaloendelea ndani kwa ndani baina ya vyama tofauti, baina ya vyama na shirikisho na baina ya shirikisho na taasisi nyingine za kiutendaji.

Kuhusu maudhui ya filamu zinazotengenezwa na wasanii wa Tanzania, Waziri Mkuu alisema inashangaza kuona masuala ya mapenzi yanaongoza kwenye filamu za Kitanzania kwa kushika nafasi ya kwanza ikiwa ni sawa na asilimia 68, ikifuatiwa na vichekesho ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa sawa na asilimia 12.

“Je, wote ni lazima muigize masuala la mapenzi kwenye filamu zenu au huwa mnaambiana mtoe maudhui yanayohusu mapenzi. Je, ni kweli kwamba Watanzania wengi wanapenda kuangalia mambo ya mapenzi?”

“Ni lazima muangalie maudhui yenu na mpanue wigo. Kwa kuwa mna shirikisho, ni vema mkagawana maeneo ya kuigiza ili kupanua soko na mkiingiza filamu zenu sokoni, zote zipate mashabiki.”

Alisema nafasi ya tatu kwenye maudhui imechukuliwa na filamu za masuala ya utamaduni na mambo ya uchawi ambayo ni sawa na asilimia 10 huku nafasi ya nne ikichukuliwana na filamu zinazohusu mapigano ambazo ni sawa na asilimia saba. “Hizi ni chache kwa sababu zinahitaji mtaji mkubwa wakati wa kuzitengeneza na pia ni risky,” alisema.

Wakitoa maoni yao ni kwa nini tasnia ya filamu imedidimia, wasanii hao ambao waliwakilisha wenzao kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Katavi na Rukwa, walidai kwamba Bodi ya Filamu imeua tasnia hiyo kwa hiyo hawana imani na Bodi na hawako tayari kufanya nayo kazi.

Waliomba pia kuwe na taratibu za kuvutia wawekezaji kwenye tasnia hiyo, uwekwe mkakati wa haraka wa kuinua soko la filamu kupitia lugha ya Kiswahili ambayo walisema ni bidhaa adimu. Pia waliomba sera ya filamu nchini ikamilishwe haraka ili iweze kulinda maslahi ya wasanii wa filamu.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Share To:

msumbanews

Post A Comment: