Sunday, 7 April 2019

MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA, UNYANYASAJI WA KIJINSIA VYATAJWA KUZOROTESHA ELIMU SEKONDARI MUHEZA

 MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati wa  kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika mjini humo. kushoto ni Diwani wa kata ya Potwe Rashid Mdachi na Afisa Elimu Msingi wilaya ya Muheza
  Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Muheza Julitha Akkho wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya elimu sekondari kwenye kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika mjini humo.
Afisa Elimu Msingi wilaya ya Muheza akizungumza katika  kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika mjini humo.
 MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo kulia akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake Diwani Kata ya Mbaramo Makame Seif wakati wa halfa hiyo
 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Muheza Like Gugu kulia akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake kwenye sekta ya elimu Meneja wa Benki ya NMB wilayani Muheza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo
 MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo kushoto akiteta jambo na maafisa elimu wilayani humo kushoto ni Afisa Elimu Sekondari wilaya hiyo Julieth Akko kulia ni Afisa Elimu Msingi wilayani humo
MATUMIZI ya dawa za kulevya, Unanyasaji wa kijinsia ikiwemo wanafunzi kupewa ujauzito vimetajwa kuwa vikwazo vikubwa kwa elimu ya sekondari hususani kwa shule za Serikali wilayani Muheza kutokuwa ya kuridhisha.

Hayo yalisemwa  na Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Muheza Julitha Akkho wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya elimu sekondari kwenye kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika mjini humo.

Alisema licha ya hivyo lakini utoro wa rejareja ambao umepelekea wanafunzi wengi kukosa masomo na kuchangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo tofauti na miaka ya nyuma.

“Ndugu zangu sisi kama wilaya ya Muheza tunakumbuka wakati wa miaka ya nyuma tulikuwa kinara kwenye suala la elimu lakini sasa tunashuka na kubwa ni changamoto zinazotukabili kwa sasa likiwemo la Mimba, Unyanyasaji wa Kijinsia”Alisema Afisa Elimu huyo.

Aidha alisema tatizo jingine ambalo linachangiwa kuwepo kwa hali hiyo inatokana na mila na desturi potofu kwa jamii wilayani humo hatua ambayo inakwamisha ndoto za wanafunzi wengi kupata elimu ambayo ingeweza kuwasaidia kwenye maisha yao na sasa na baadae.

Akizungumzia tatizo la wanafunzi kupata ujauzito wilayani humo Afisa elimu hiyo alisema hali imekuwa sio ya kuridhisha kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata mimba kwa shule za Sekondari.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zinaonyesha kwamba ongezeko hilo limetoka mimba 24 mwaka 2017 hadi kufikia 35 mwaka 2018 huku mwaka 2019 kufikia machi zikiwa zimepatikana mimba 4 huku kwenye suala la utoro sekondari ni 2017  wanafunzi 332 na mwaka jana wakipatikana
watoto 220.

Awali akiwasilisha taarifa ya Tahosa wilayani humo Mwakilishi wa Tahosa wilaya ya Muheza George Kaunda alisema changamoto kubwa ni upungufu wa vitabu vya kiada katika masomo ya sanaa ambayo ni uraia,Historia na Geografia na kufanya kazi kuwa ngumu ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kaunda ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Mtindiro wilayani Muheza alisema changamoto nyengine ni utoaji wa huduma ya chakula shuleni bado ni tatizo kutokana na wazazi na walezi kuwa na mwitikio mdogo kwenye kuchangia na kufanya wanafunzi wengine kwenye
baadhi ya shule kutokula chakula na kupelekea kuwa ngumu katika ufundishaji hususani katika vipindi vya mchana na vipindi vya watoto kuelewa kuwa chanzo cha kutokufanya vizuri kimasomo darasani.

Akizungumzia suala la miundombinu ambapo alisema asilimia 90 kuna mapungufu makubwa kwa mfano mapungufu ya vyumba vya madarasa, shule nyingi hakuna majengo ya utawala, nyumba za walimu, matundu ya vyoo kwa walimu na wanafunzi kwa baadhi ya shule.

“Lakini pia vilevile katika shule zetu kuna maboma ya vyumba vya walimu, madarasa pamoja na vyumba vya maabara ambavyo bado vinahitajika umaliziaji, samani pia kuna changamoto kubwa ya viti na meza za walimu hatua inayosababisha walimu kufanya maandalizi ya ufundishaji wakiwa wamesimama”Alisema.

Naye kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo
alisema elimu ilianzisha wilayani muheza lakini wakaona inataka kuporomoka hali iliyopelekea kukukata na wadau huku wakiweka mipango kabambe ya kuanzisha kampeni mbalimbali za kusaidia sekta hiyo.

“Lakini pia kuna kundi maalumu lililosahaulika la watoto wenye mahitaji maaluimu watoto yatima wanakosa mahitaji japokuwa wana uwezo mkubwa shuleni….pia watoto wenye ulemavu aina mbalimbali wana haki ya kusoma lakini miundombinu sio rafiki kwao ndio tukafanya kampeni ya
kukusanya fedha kwa ajili ya miundombinu na vifaa vyao”Alisema DC Mhandisi Mwanasha .


Mwisho.

No comments:

Post a comment