Maelfu ya wajane leo wamefurika ukumbi wa Mlimani City kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda wa kusikiliza kero za wajane ambapo ametoa ahadi ya kupigana usiku na mchana kuhakikisha waliodhulumiwa mirathi wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria.

RC Makonda amesema moja ya mambo yanayomnyia usingizi ni vilio vya kinamama wajane ambao wamedhulumiwa Mali walizochuma na waume zao enzi za uhai jambo linalopelekea wengi wao kuishi maisha ya tabu.

Aidha RC Makonda amesema kupitia kongamano hilo limemsaidia kujua ukubwa wa tatizo la wajane katika Mkoa wake na kinachofuata ni kuandaa jopo la wataalamu wa sheria watakaopitia fomu zilizojazwa na kila mjane kisha kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kandamizi kisha kwa wajane na kuziwasilisha kwa waziri wa sheria.

Katika hatua nyingine RC Makonda amepokea Ripoti ya kamati aliyoiunda kufuatilia sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa ambayo ndani yake imebaini uwepo wa changamoto kubwa ikiwemo kukosekana kwa malezi ya mtoto,ubakaji,kulawiti na kukosekana kwa mfumo mzuri wa utoaji haki.

Pamoja na hayo RC Makonda amewasihi wajane wasijione wanyonge na badala take wajitume kwenye kutafuta kipato cha familia huku akiwahimiza kusimama imara katika suala la malezi ya watoto.

Katika Kongamano hilo Wajane wamejengewa uelewa wa mambo mbalimbali waliyokuwa hawayafahamu katika nyanja za sheria, Mirathi, Malezi na namna ya kujikwamua kiuchumi kupitia fursa ya mikopo ya fedha bila riba inayotolewa na manispaa.
Share To:

Post A Comment: