Wednesday, 17 April 2019

LUKUVI AONYA WENYEVITI WA MITAA MAUZIANO YA ARDHI


 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Wakazi wa Kikwajuni Vijibweni wilaya ya Kigamboni alipokwenda kutatua mgogoro kati ya Mwekezaji Registered Trustees Korea Church Mission  jijini Dar es Salaam jana.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi  akitembea kuelekea eneo lenye mgogoro kati ya Wananchi wa Mkwajuni Vijibweni wilaya ya Kigamboni maarufu kama kwa Mkorea na Mwekezaji wakati alipokwenda kutatua mgogoro katika eneo hilo jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza mwananchi wa Mkwajuni Vijibweni  Mariam Kange alipokwenda kuatatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa eneo hilo maarufu kwa Mkorea na Mwekezaji Registered Trustees Korea Church Mission (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta
Waziri wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William lukuvi amewaonya wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutojihusisha na masuala ya uuzaji ardhi katika maeneo mbalimbali kwa kuwa hapaswi kisheria kufanya kazi hiyo.
Lukuvi alitoa onyo hilo jana wakati alipokwenda kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kikwajuni Vijibweni maarufu kama kwa Mkorea wilayani Kigamboni mkoa wa Dar es Salaam na Mwekezaji  ‘Registered Trustee of Korea Church Mission’ katika eneo hilo la ukubwa wa ekari 305.
Lukuvi alisema sheria ya ardhi haisemi kama wenyeviti wa mitaa wanaruhusiwa kusimamia uuzaji ardhi na kusisitiza kuwa wenyeviti hao hawana mamlaka ya kufanya hivyo na mwenye jukumu la kusimamia masuala ya ardhi katika miji ni halmashauri za mji au Manispaa.
Waziri wa Ardhi alisema mtu yeyote atakayeuziwa ardhi kupitia wenyeviti hao wa mitaa au mtu mwingine asiyetambuliwa kisheria basi atakuwa ameuziwa ‘bomu’ na kuwataka wananchi kuwa makini na suala hilo na kuwashauri kabla ya kununua eneo lolote ni vyema wakaiuliza mamlaka husika iwapo eneo husika limepangwa kwa matumizi ya aina gani ili kuepuka kubomolewa.
‘’Ukitaka kununua kiwanja kwanza kaulize Manispaa maana unaweza kununua eneo kumbe ni la kuzikia kwani manispaa ndiyo inayojua kama eneo hilo ni salama’’ alisema Lukuvi
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi ametoa siku kumi kwa halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kufanya uhakiki kwa wananchi wote wanaoishi eneo lenye mgogoro na Mwekezaji la Kikwajuni Vijibweni Kigamboni maarufu kwa Mkorea ili kupata taarifa sahihi za wananchi hao.
Aidha, amemtaka Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam Methew Mhonge kupata nakala ya hukumu ya kesi ya wananchi hao dhidi ya Mwekezaji ‘Registered Trustees Korea Church Mission’ inayoonesha kuwa wananchi wa eneo hilo wameshindwa kesi na wanatakiwa kuondoka.
Maagizo hayo ya Lukuvi yanafuatia kuelezwa na wananchi 22 wa Kikwajuni kupitia mwakilishi wao Meja Mstaafu Peter Ismail kuwa haki haikutendeka wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo hilo jambo lililosababisha kukataa kuchukua fidia na wengine 6 kudai nyongeza ya fidia huku wananchi 95 wakilalamika.
Meja Mstaafu Ismail alisema, wao walichukua uamuzi wa kutokubaliana na mwekezaji aliyetaka kuwafidia laki nne kwa ekari moja wakati wao walitaka kulipwa shilingi milioni moja kwa ekari moja na kufafanua kuwa kilichowashangaza ni Mwekezaji kulipa fidia mwaka 2015 wakati zoezi hilo lilitakiwa kufanyika miezi sita baada ya Agosti 2004.
Kwa upande wa wananchi sita wanaotaka kuongezewa fidia wananchi hao kupitia mwakilishi wao Hamza Rashid walidai kesi yao iliamuliwa kupatiwa taarifa halisi ya uthamni na siyo nakala kama walivyofanyiwa jambo walilolieleza kuwa halikufanyika.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Lukuvi aliagiza taarifa zote muhimu zipatikane kipindi cha siku kumi ikiwemo Mwekezaji kuwasilisha mpango wa jinsi atakavyolitumia eneo hilo la ekari 305 sambamba na chanzo cha mtaji wa uwekezaji huo.
Eneo la Kikwajuni Vijibweni maarufu kwa Mkorea kwa muda mrefu tangu mwaka 2004 limekuwa na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa eneo hilo na Mwekezaji ‘Registered Trustees Korea Church Mission’ anayetaka kujenga chuo Kikuu.

No comments:

Post a comment