DSC_5008-min
Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga cha Mji Mwema, Kigamboni wakikarabati mlango wa chumba cha leba cha  Zahanati ya Mji Mwema. Mwishoni mwa wiki
DSC_5043-min
Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga wakifanya usafi wa eneo la mtaro wa maji machafu kwenye Zahanati ya Mji Mwema, Kigamboni mwishoni mwa wiki.
DSC_5226-min
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mji Mwema, Dk. Beno Constatino, akitoa mkono wa pongezi kwa Vijana wa kikundi cha Gonga Gonga, muda mfupi baada ya kumaliza shughuli za ukarabati na usafi wa mazingira wa Zahanati hiyo, mwishoni mwa wiki.
DSC_5051-min
Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga cha Mji Mwema, Kigamboni wakifanya usafi cha choo  cha wagonjwa cha Zahanati ya Mji Mwema. Mwishoni mwa wiki (Picha na Andrew Chale
…………………………..


NA Andrew Chale

KIKUNDI cha Gonga Gonga kinachojishughulisha na shughuli za useremal, wamejitolea kufanya ukarabati na usafi katika Zahanati ya Mji Mwema, iliyopo wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

Kikundi hicho kiliweza kutengeneza milango iliyokuwa inasumbua ikiwemo ya vyoo, vyumba vya madaktari na maeneo mengine huku pia wakirekebisha vifaa vya umeme ikiwemo feni za majengo hayo.

Mbali na kufanya ufundi mdogomdogo pamoja na kuweka vifaa vipya, vijana hao walifanya usafi wa mazingira ikiwemo kufyeka majani na kuzibua mtaro wa maji machafu uliokuwa maeneo ya zahanati hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Katibu wa Gonga Gonga, Ali Rajab Ali, alishukuru kwa nafasi waliyopewa na uongozi wa zahanati hiyo na kusema walichofanya ni kuonesha kuunga mkono juhudi mbalimbali katika jamii.

“Tunashukuru kwa kupewa nafasi ya kufanya tukio hili, kwani lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunawatoa kwenye msongo wa kufikiria kifaa fulani hakifanyi kazi ama mlango haifungi.

Kwa umoja wetu pia tumefanya usafi wa mazingira maeneo yote yanayozunguka zahanati” alisema Ali.

Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mji Mwema, Dk. Beno Constatino, alikipongeza kikundi hicho kwa namna walivyojitolea kufanya shughuli za kijamii kwenye zahanati hiyo huku akiwaomba kuwa na utaratibu huo mara kwa mara.

Dk. Beno alisema awali walikuwa wanapata changamoto kwenye hasa milango ukiwemo mlango wa leba.

Dkt. Beno alibainisha kuwa, awali walikuwa wanapata changamoto kwenye mlango huo wa leba na hata walikuwa wakiamua kusafirisha mgonjwa kuhamishiwa kituo cha Vijibweni.

Nae Mwenyekiti wa Gonga Gonga, Seleman Omari amesema wameamua kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali hivyo kujitolea kwao huko ni kuungana na Rais katika kauli yake ya Hapa kazi.

“Tunaungana na Serikali kuhakikisha kazi zinafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa madaktari na wauguzi ama wagonjwa wanaofika hapa kuwa mazingira salama.

Kwa ujuzi wetu wa ufundi tumejitolea kufanya shughuli hii bure kabisa kwani inawasaidia ndugu zetu na pia hata sie wenyewe” alisema Omari.

Aidha, Omari aliongeza kikundi hicho cha Gonga Gonga kimesajiliwa kisheria na kipo toka mwaka 2005 wakiwa vijana sita na baadae kuhamasishana na sasa kufikia 22 ambapo wanashughulika na ufundi mkubwa wa useremala, Sanaa za vitu vya uselemala, Umeme, Kilimo na mambo mengine.
Share To:

Post A Comment: