WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa viwanda kwenye mkoa wa Tanga kwa sababu vitasaidia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.

Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Novemba 1, 2018) alipotembelea kiwanda cha saruji cha Rhino na kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh, vyote vya jijini Tanga.Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, aliwapongeza wawekezaji wa viwanda hivyo kwa kuunga mkono mkakati wa Serikali. 

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.Akizungumzia kuhusu kiwanda cha Rhino, Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho na vingine vya saruji nchini vitasadia kupunguza gharama ya saruji nchini na kurahisisha ujenzi.

“Serikali inaamini kwamba uwepo wa viwanda mbalimbali nchini si tu utawezesha ukuaji wa uchumi wa Taifa, pia utasaidia katika kumaliza changamoto ya ajira hususani kwa vijana.”Akiwa katika kiwanda cha Tanga Fresh, Waziri Mkuu aliwataka wafugaji mkoani Tanga wabadili mfumo wa ufugaji na wafuge kwa kutumia njia za kisasa ili waongeze uzalishaji.

“Wafugaji lazima wakubali kubadilika watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hiki kwa kufuga kisasa ili wapate maziwa mengi kwa sababu wana uhakika wa kuyauza kiwandani hapa”.Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wananchi walioajiriwa kiwandani hapo wafanye kazi kwa bidii, uaminifu na wawe waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya wizi kwa kuwa havina tija.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, NOVEMBA 2, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu uzalishaji wa saruji  kutoka kwa Bw. Pradeep Punlana  (katikati) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha saruji cha  Rhino kilichopo eneo la Maweni jijini Tanga  wakati alipotembelea kiwanda hicho  Novemba 1, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu uzalishaji wa saruji  kutoka kwa Bw. Pradeep Punlana  (katikati) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha saruji cha  Rhino kilichopo eneo la Maweni jijini Tanga  wakati alipotembelea kiwanda hicho  Novemba 1, 2018


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama usindikaji wa maziwa wakati alipotembelea kwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh cha jijini Tanga, Novemba 1, 2018.  Kushoto ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, watatu kushoto ni Meneja Ufundi wa kiwanda hicho, Adam Gamba na wanne kukhoto ni Meneja Mkuu wa kiwanda, Michael Karata. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Soni wilayani  Lushoto akiwa katika ziara ya mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Share To:

msumbanews

Post A Comment: