Sunday, 12 August 2018

Vijana wafanya kongamano jijini Arusha


Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya vijana duniani, vijana wamekutana pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana ili kujadili mambo yanayohusu vijana nchini.

Lengo la kongamano hilo ni kujadili masuala ya kimaendeleo kwa vijana na changamoto zinazowakabili ili waweze kuzitatua kwa pamoja na kufikia malengo waliyokusudia.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi mdogo wa mkutano wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Richard Kwitega alisema kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwawezesha vijana ili waweze kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa maendeleo ya Taifa.


“Vijana wana nafasi kubwa katika jamii na kama watatumia vizuri majadilano haya wanaweza kupata mbinu mpya zitakazosaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la ajira kwa kuazisha shughuli za uzalishaji mali ili waweze kukua kiuchumi” alisema Kwitega.

Naye Afisa wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Eliakim Mtawa ameeleza kuwa majadiliano haya yatawajengea vijana uwezo ikiwemo maborosho ya Sera ya vijana iendane na wakati wa sasa na ushirikishwaji wa vijana katika fursa mbalimbali katika jamii.

“Kongamano hili la vijana litasaidia kubadili mfumo wa vijana kwa kutambua wao ndio nguvu kazi inayotegemewa na Taifa, hivyo ni vyema wakatumia vizuri fursa zilizopo kwa kujiendeleza kiuchumi” alisema Mtawa.

Aliongeza pia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na program ya ukuzaji ujuzi nchini ambapo vijana wengi wameweza kunufaika kwa kuwezeshwa kiuchumi na kuweza kujiajiri na kuajiri wenzao kupitia vikundi ya ushirika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa AfriYAN Tanzania Bi. Dianarose Lyimo alisema kuwa majadiliano haya yatawasaidia vijana kuwa na maadhimio watakayokubaliana kwa pamoja kama vijana kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana kutambua mawazo na mchango wa vijana.

Kongamano hili la vijana limehusisha wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu (Idara ya Maendeleo ya Vijana), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, TAKUKURU, Wizara ya Fedha, UMATI, Pathfinder International, DSW Tanzania, UNICEF, UNFPA, Hope for Young Girls, Vision for Youth, Salama Foundation, Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitolea (VSO), Restless Development, AfriYAN Tanzania, HIEFER International, Jitegemee Vijana Tanzania Foundation, OKOA Mtaa – Monduli, Shujaaz, Voice of Youth Tanzania na  Halmashauri ya Wilaya ya Meru.

No comments:

Post a comment