Sunday, 12 August 2018

MASHINDANO YA ANGELINE JIMBO CUP 2018 YAZINDULIWA RASMI

Mashindano ya mpira wa miguu yanayojulikana kama   Angeline Jimbo Cup 2018 yamezinduliwa rasmi hii leo Agosti 11, 2018 katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza yakitarajiwa kukutanisha Timu za Vijana kutoka kata 19 za Jimbo la Ilemela yenye kauli Mbiu ya 'Michezo ni  Ajira' .


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni rasmi ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Severine Lalila mbali na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuanzisha na kuendeleza mashindano hayo, amewataka wananchi wa wilaya ya Ilemela kutumia michezo kama sehemu ya kujiingizia kipato lakini pia kudumisha umoja na mshikamano walionao huku akitaja baadhi ya wachezaji wenye mafanikio makubwa baada ya kujiajiri kupitia michezo akiwemo Mbwana Samatta anaecheza mpira wa kulipwa nchini Ubeligiji akitokea Tanzania

‘…  Ndugu zangu michezo hii ni afya lakini pia ni ajira, Kama mnavyojua tunao vijana wanaotutangaza duniani kama kina Mbwana Samatta, Naamini kupitia mashindano haya ya mheshimiwa Mabula upo uwezekano wa kupata kina Samatta wengine ..’


Aidha Mhe Dkt Severine amewaasa wachezaji wa Timu zote zinazoshiriki mashindano hayo kuhakikisha wanazingatia sheria 17 za mpira wa miguu pamoja na kuwa na nidhamu kwa waamuzi na wakufunzi wao ili kuzipatia ushindi Timu zao.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ambae pia ndio muasisi na mdhamini mkuu wa mashindano hayo amesema kuwa mashindano ya Jimbo Cup yamelenga kuibua vipaji vipya vinavyopatikana ndani ya jimbo lake lakini pia kuvikuza vile vya zamani huku akiwahakikishia kuwa mashindano hayo yatafanyika kila mwaka mara baada ya kupatikana Timu shiriki kutoka ngazi ya kata pamoja na kuwaomba viongozi na wananchi wa jimbo hilo kuunga mkono jitihada anazozichukua katika kuhakikisha wilaya ya Ilemela inaendelea kuwa tanuru la kuoka na kuzalisha vipaji vya michezo mbalimbali nchini sanjari na kutaja baadhi ya wachezaji waliotokea jimbo la Ilemela  akiwemo Jerry Tegete, Mrisho Ngasa, Mbui na wengineo wanaocheza katika vilabu mbalimbali kwa sasa wakitokea Mbao Fc yenye makazi yake Ilemela.


Mashindano ya The Angeline Ilemela Jimbo Cup yalitanguliwa na zoezi la kukabidhi vifaa vya michezo kwa Timu zote zinazoshiriki ligi hiyo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo na baadae mchezo wa ufunguzi uliozikutanisha Timu ya kata ya Kirumba dhidi ya Timu ya kata ya Ibungilo ambapo Timu ya kata ya Kirumba imepata kichapo kikali cha kufungwa goli moja kwa sifuri lilifungwa na mchezaji wa kata ya Ibungilo aliyejulikana kwa jina la Ally Ally katika kipindi cha pili.

Mashindano haya yatakuwa yakiendelea kwa siku tofauti tofauti katika viwanja vya Kona ya Bwiru, Magomeni, CCM Kirumba, Sabasaba, na Bugogwa shule ya msingi.

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
11.08.2018.

No comments:

Post a comment