MWENYEKITI wa Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Kheri James amewataka vijana wasomi nchini kuhakikisha tija ya elimu waliyonayo inanufaisha jamii iliyowazunguka kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Rai hiyo aliitoa wakati akiwahutubia vijana waliofaulu mtihani wa kidatu cha sita kwa daraja la kwanza, la pili na tatu  (Division I,II na III) mwaka 2018 Zanzibar huko katika ukumbi wa Z-ocean iliyopo Bububu Wilaya ya Magharibi ‘’A’’  Zanzibar.

Alisema endapo vijana hao watashindwa kuzitumia vizuri elimu zao kwa kuzinufaisha jamii zilizowazunguka basi elimu hizo zitakuwa hazina maana kwao wao na taifa kwa ujumla.

Alisema serikali zote mbili ambazo ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendelea kuthamini vijana kwa kuwawezesha kupitia nyanja mbali mbali hasa za kitaaluma.


Aliwataka vijana hao ambao watajiunga na elimu ya juu katika vyuo mbali mbali nchini kuwa wanatakiwa kusoma masomo ambayo wana uwezo nayo ili waweze kufaulu vizuri katika masomo ya elimu ya juu na wawe wataalamu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Mwenyekiti huyo Kheir alifafanua kwamba CCM na serikali zake mbili inawaamini vijana kwa kuwapatia nafasi mbali mbali za uongozi sio kwa sababu za kujuana bali ni kutokana na sifa walizokuwa nazo kitaaluma.

“ CCM haina vijana wa ovyo ovyo kama zilivyo taasisi zingine za kisiasa bali ina vijana madhubuti, wazalendo,weledi na wenye sifa na kila vigezo vinavyokubalika katika nyanja mbali mbali za uongozi na utendaji katika taasisi za serikali na binafsi.”alifafanua Mwenyekiti huyo.

Alisema taasisi yoyote isiyokuwa na utaratibu wa kurithisha uongozi kutoka kizazi kimoja kwenda kingine basi taasisi hiyo itakuwa ni sawa na mfu na ndio maana CCM inaendeleza utaratibu wa kuwarithisha na kuwaanda vijana wake kiungozi ili waweze kuwa viongozi bora ndani na nje ya Serikali zao.

Alieleza kuwa suala la vijana kupendana ni lazima na sio hiari kwani endapo kundi hilo litaendekeza tabia ya kufanyiana fitna, majungu na kuchafuana hawatokuwa na uwezo wa kulinda rasilimali za taifa kwani nguvu nyingi watakuwa wanazitumia kuchafuana badala ya kufanya mambo ya maendeleo.

Pia aliwataka viongozi wa serikali kuendeleza utamaduni wa kusema na kutangaza mambo mema yanayofanywa na serikali kwa wananchi pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayopotoshwa na baadhi ya watu wasioitakia mema CCM na serikali zake.

Pamoja na hayo aliwambia viongozi vijana walioaminiwa na kupewa nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali wafanye kazi zao kwa uadilifu ili vijana na wananchi kwa ujumla waendelee kuwaamini na kujifunza mambo mema kutoka kwao.

Mwenyekiti huyo alikemea vikali tabia za baadhi ya vijana wanaopenda kulalamika bila ya kujituma kufanya kazi kwa kubuni mambo mbali mbali ya kuwaingizia kipato pamoja na kulitumikia taifa kwa maendeleo endelevu.

Kupitia mkutano huo aliipongeza CCM Zanzibar kwa juhudi zake  za kuendeleza utamaduni wa kuwaamini vijana wasomi kwa kuwapatia fursa mbali mbali zinazowasaidia kupata elimu ya juu na mafunzo ya ujasiriamali bila ya usumbufu.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla (Mabodi) alisema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kulea kitaaluma vijana wa makundi yote ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi.

Alisema CCM Zanzibar inatekeleza mipango mbali mbali ya kuwawezesha vijana kwa kuwajengea mazingira bora yatakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kuwasaidia vijana wenzao ambao bado hawajafika ngazi ya elimu ya juu.

 Pia alieleza kwamba taasisi hiyo pia inaendelea na mikakati ya kuanzisha miradi mikubwa ya ujasiriamali itakayowezesha vijana ambao hawakufika elimu ya juu kuweza kujiajiri wenyewe.

“Chama chetu kinajali vijana wa makundi yote na sio wasomi pekee na ndio maana mipango yetu ya kuwajengea uwezo ipo kwa vijana wa makundi yetu na ndio maana hata nchi yetu imekombolewa na vijana waliokuwa wakwezi na wakulima.”, alisema Dk.Mabodi.

Mapema Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita alisema vijana hao wapo tayari kutumia uwezo wao wote kulinda na kuthamini mambo mema yanayotekelezwa na Serikali zote mbili chini ya usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi.

Sherehe hiyo imeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kwa kushirikiana na UVCCM  kwa lengo la kuwapongeza vijana 470 wa kidato cha sita Zanzibar waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, pili na tatu (Division I,I na III) mwaka 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: