Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA imezindua rasimu ya mkataba kwa wateja sambamba na kampeni ya kupambana na rushwa ndani ya mamlaka hiyo.

Lengo la rasimu hiyo ni kuweka ufanisi na uwazi katika kazi za mamlaka hiyo.

Jana Jumatatu Julai 16, 2018 Mkurugenzi wa TCRA, mhandisi James Kilaba alisema mkataba huo utabainisha viwango vya utoaji huduma kwa wateja na haki na wajibu wa wateja kulingana na huduma zinazotolewa.

Alisema TCRA itatumia mkataba huo kama nyenzo muhimu ya kuzuia na kupambana na rushwa  kama inavyopewa uzito na Rais John Magufuli.

“Ndani ya mkataba huu tutawaonyesha wateja huduma tunazotoa, viwango vya hudumana uhusiano kati ya watumishi na wateja. Mkataba huu pia unalenga kuongeza tija na uwajibikaji kwa watumishi wa TCRA katika kutoa huduma bora kwa wateja wetu,"alisema.

Alibainisha kuwa hatua hiyo itawezesha dhamira ya ukweli na uwazi katika kazi zao kutimia, kubainisha kuwa kutimia kwa dhamira hiyo  itakuwa kinga ya kuzuia malalamiko ambayo yanaweza kutafsiriwa na wananchi kuwa ni vitendo vya rushwa.

“Upatikanaji wa habari sahihi bila vikwazo utaongeza uwazi na uwajibikaji wa kila mtumishi na hivyo itapunguza malalamiko,” alisema na kwamba mkataba huo utaendelea kuboreshwa kulingana na mahitaji ya utoaji huduma.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: