Friday, 20 July 2018

Ndalichako aingilia kati sakata la Jangwani

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA, PROF. JOYCE NDALICHAKO.

MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, yamezidi kuwa gumzo na hata kuonyesha kuwatahayarisha viongozi huku Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akitoa tamko zito.

Kutokana na matokeo hayo, Waziri Ndalichako amewaonya maofisa elimu, wadhibiti ubora na wakuu wa shule nchini wasiosimamia kikamilifu elimu, wataondolewa kwenye nafasi zao.

Prof. Ndalichako alitoa onyo hilo jana wakati wa hafla fupi ya kukabidhi magari 47 kwa wathibiti ubora wa elimu nchini iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) jijini hapa.

Katika matokeo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita, shule hiyo kongwe nchini ilikuwa moja ya shule 10 zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo. Katika matokeo hayo, shule hiyo ilishika nafasi ya 451 kati ya 453 zilizofanya mtihani huo.

Prof. Ndalichako alisema viongozi na wasimamizi wa shule wanapaswa kuwajibika kwa kushindwa kusimamia taaluma na nidhamu kwa wanafunzi.

Alisema licha ya shule hiyo kuwa na walimu wa kutosha na kupatiwa vifaa vya taaluma vya kutosha, usimamizi mbovu, utoro wa walimu na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi vimechangia shule hiyo kushika mkia katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita.

"Tatizo lililopo pale (Jangwani) ni usimamizi, kwa sababu walimu wako 87 kwa hiyo huwezi kusema ina tatizo la walimu. Vifaa vipo vya kutosha na wakati mwingine hatusemi imekuwa ikipokea vifaa vya ziada kulinganisha na mgawo wa kawaida, lakini inakuwa shule ya mwisho,” alisema.

 Aliongeza kuwa walimu wengi katika shule hiyo wamekuwa wakitia saini vitabu vya mahudhurio na kuondoka, huku mratibu wa elimu kata akiwa amekaa tu hadi shule inakuwa ya mwisho.Matokeo kama hayo yakitokea kwa shule zingine, alisema watendaji hao kama wataendelea kushindwa kusimamia elimu, wataondolewa kwenye nafasi hizo kwa kushindwa kuwajibika kikamilifu.

“Elimu ni kila kitu, hakikisheni mnasimamia elimu ili kutengeneza watu walioelimika na kuleta mageuzi ya kiuchumi katika nchi,” alisema Prof. Ndalichako.

Ndalichako alisema serikali itaendelea kuwapima uwezo wao wa kazi kutokana na matokeo ya mitihani ya kitaifa itakayokuwa ikifanyika kila mwaka.

Alisema magari hayo 47 yaliyotolewa na serikali ni kwa ajili ya wadhibiti ubora wa elimu nchini na yasitumike kwa ajili ya kazi zingine katika halmashauri nje ya elimu.

Alibainisha kuwa serikali imeanza kutoa vitendea kazi na kwamba hivi karibuni ilitoa pikipiki 2,894 kwa ajili ya waratibu wa elimu kata kwa nchi nzima, ili kufanya kazi katika maeneo yao ya utawala.

Aliongeza kuwa serikali imejenga mabweni, madarasa na kukarabati baadhi ya majengo ya shule kongwe 45 pamoja na vyuo vya ualimu.

Sambamba na ukarabati huo wamejenga mabweni 129 na kununua vifaa vya masomo ya sayansi, ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.

Upande wa Wakuu wa Shule, Waziri Prof. Ndalichako aliwaagiza kusimamia sheria na taratibu za shule pamoja na nidhamu ya kila mwanafunzi na wasitumie simu wakiwa shuleni.

Aliwataka kuwasimamia walimu wanaofundisha katika shule zao na kuhakikisha wanaingia darasani kufundisha na si kupiga hadithi na wanafunzi.

“Kuna mabadiliko ya elimu nawaomba kila mtu katika nafasi yake atekeleze majukumu yake ili kuleta mafanikio, mwanafunzi asome kwa bidii na walimu waingie darasani kufundisha,” alisema Waziri Ndalichako.

Pamoja mafanikio hayo, Prof. Ndalichako alisema wizara hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa walimu na utoshelevu wa miundombinu katika shule na vyuo.

Naye Mkaguzi wa Udhibiti wa Ubora wa Shule Tanzania, Efranzia Buchuma, alisema magari 45 yatapelekwa katika halmashauri mbalimbali nchini na magari mawili yatapelekwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Buchuma aliishukuru serikali kwa kutoa vitendea kazi hususan magari kwa wadhibiti ubora wa elimu na kuahidi kuwa watakwenda kufanya kazi kwa bidii, ili kuboresha kiwango cha elimu

No comments:

Post a comment