Friday, 1 June 2018

Wachezaji wa Singida United kila mmoja apewa mifuko 50 ya Saruji


KLABU ya Singida United, kesho Jumamosi inatarajiwa kumtangaza rasmi kocha wake mkuu atakayechukua mikoba ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm, aliyetimkia Azam FC, lakini habari nzuri kwa wachezaji wa timu hiyo ni kwamba kila mmoja wao amepewa mifuko 50 ya saruji.

Wakati Singida ikitarajiwa kumtangaza kocha huyo katika mchezo wao kesho Jumamosi wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, jana Alhamisi iliwatambulisha nyota wake wapya watatu ambao wataanza kuonekana katika michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza keshokutwa Jumapili nchini Kenya.

Singida imetangaza rasmi kuwa msimu ujao haitakuwa na Pluijm ambaye anajiunga na Azam FC hivyo anayechukua mikoba yake atatambulishwa baada mechi hiyo ya Kombe la FA na atakabidhiwa mikoba rasmi kwa ajili ya michuano ya SportPesa Super Cup.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema wachezaji hao watatu waliowachukua ni straika Mbrazili, Fellipe Oliveira da Santos na viungo Amara Diaby na Tiber John.

“Baada ya mechi ya fainali ya FA siku ya Jumamosi, ndipo kocha mpya atatambulishwa baada ya Pluijm kumaliza majukumu yake kwenye mchezo huo, kocha huyo mpya ndiye atakayeenda na timu kwenye michuano ya SportPesa Super Cup.

“Na suala la kiungo Mudathir Yahya bado tunaendelea kuweka mambo sawa na mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuendelea kubaki hapa, hivyo mambo yakikamilika mtafahamu.

“Pia wachezaji wa klabu yetu wamepewa zawadi kila mmoja ya mifuko 50 ya saruji kutokana na juhudi pamoja na kupambana mpaka kuifikisha timu hapa ilipo,” alisema Sanga.

No comments:

Post a comment