Mlinda Mlango wa klabu ya Mtibwa Sugar, Benedicto Tinocco, ameibuka na kuzungumzia machache kuhusiana na taulo lake ambalo amekuwa akiliweka langoni wakati wa mchezo wa dhidi ya timu pinzani.

Kipa huyo ambaye aliwahi kusajiliwa Yanga na kisha kuelekea Mtibwa, amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakilichukulia taulo hilo kama sehemu ya imani potofu za kishirikina jambo ambalo ameeleza si kweli.

Kwa mujibu wa Spoti Xtra ya Clouds FM, Tinocco amesema taulo hilo halina kazi nyingine zaidi ya kufutia majasho wakati mechi ikiendelea Uwanjani sababu mikikimikiki ambayo inamlazimu atokwe na majasho.

Kauli hiyo imekuja kutokana na baadhi ya mashabiki na hata wadau wa mpira kumtilia mashaka juu ya taulo hilo.

"Unajua watu wamekuwa wakinitilia mashaka juu ya taulo langu napokwenda nalo Uwanjani wakidhani kuwa linazuia magoli, hilo halina ukweli kwani kazi yake ni kufutia majasho pekee tofauti na wengi wanavyodhani kuwa linahusika na masuala ya kishirikina" amesema Tinocco.

Inakumbukwa kuwa taulo hilo liliwahi kumsababishia adhabu Mshambuliaji wa Singida United, Tafadzwa Kutinyu kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu baada ya kulifuata taulo lake golini kisha kulitupilia nje akiamini linahusika na ushirikina katika mchezo ambao Singida ililala kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa ligi, Uwanja wa Namfua.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: