MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wamemtumia beki wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kufichua jezi zao za msimu ujao ambazo wanaweza kuanza kuzitumia kwenye michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya.

Simba SC wametoa picha ya Tshabalala akiwa na jezi yao mpya, ambayo imefanana mno na jezi mpya za msimu ujao za Arsenal ambazo wamezindua hivi karibuni.


Kuna tofauti kidogo tu, ambazo mtu anahitaji kutulia na kuzitazama kwa makini ili kubaini, ikiwemo ya jezi za Arsenal kuwa za kushika miili ya wachezaji na za Simba ni pana kidogo.
Simba SC imekiwshaanza kujipanga kwa msimu ujao ambao watacheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013.


Hiyo ni baada ya Wekundu hao wa Msimbazi kufanikiwa kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwapiku mahasimu wao wa jadi, Yanga SC waliokuwa mabingwa watetezi.   


Simba SC imemaliza msimu na pointi 69 baada ya mechi zake 30, ikifuatiwa na Azam FC iliyomaliza na pointi 58 mbele ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga SC walioishia kwenye pointi 52.
Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.


Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.


Timu nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: