Saturday, 2 June 2018

Naibu Waziri Akataa Bajeti ya Mil. 51 ya kujenga Mochwari ya Muriet

 Na Charles Swai, Arusha

Naibu Waziri Wa ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Josephat  Kandege Amemuagiza Mkuu Wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro pamoja na wataalamu kupitia upya andiko la bajeti ya ujenzi Wa jengo la kuhifadhia maiti cha kituo cha afya cha Muriet kutokana na kutokuridhishwa na fedha zilizotengwa kwajili ya ujenzi wa jengo hilo.

Kandege ametoa agizo hilo Leo katika ziara yake ya ukaguzi Wa hosipitali na vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa ambapo amesema kuwa hajaridhishwa na bajeti ya shilingi milioni 51 zilizotengwa kwa ajili ya jengo hilo kwani katika maeneo mengine jengo la kuhifadhia maiti limejengwa kwa shilingi milioni 24 tu.

Aidha amemuagiza Mkuu Wa wilaya kupitia bajeti hiyo na kujiridhisha hiyo milioni 51 inatumikaje ikiwa ni pamoja na kupeleka sampo ya bati lililotumika kuezeka jengo hilo TBS ili kupata uhakika  kama lipo kwenye ubora unaotakiwa  na kuweza kuepuka changamoto ya majengo ya serikali  kuchakaa baada ya muda mfupi na kuwa tofauti na gharama nyingi iliyotumika.

Amefafanua kuwa lengo la maagizo yake  ni kutaka kuhakikisha kila shilingi inayotumika inatumika kwa usahihi ambapo pia amewataka wataalamu kufanya marekebisho katika vyumba vya kujifungulia kwa kujenga vyumba visivyokuwa na mwingiliano baina ya mtu  mmoja na mwingine kwani wakinamama waliowengi wanataka wakati Wa kujifungua iwe siri yake  na muuguzi au Daktari tuu.

Sambamba na hayo amewataka  wataalamu Wa ujenzi kuhakikisha ujenzi Wa majengo ya kituo hicho cha afya pamoja na ujenzi Wa hosipitali ya wilaya unakamilika kwa muda uliopangwa  kwani wananchi wanahitaji vituo hivyo vikamilike na vianze kutumika.


Kwa upande wake Mkuu Wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro amesema kuwa wamepokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi mapema iwezekanavyo na baada ya kukamilisha watatoa taarifa.

No comments:

Post a comment