Monday, 21 May 2018

UBINGWA WA SIMBA TAIFA HAUJAWAHI KUTOKEA BONGO


Wachezaji wawili wa zamani wa Simba, Juma Kaseja na Edward Christopher, jana Jumamosi waliharibu sherehe za ubingwa wa timu yao ya zamani baada ya kuiongoza Kagera Sugar kushinda bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Taifa katika moja ya mechi za kukamilisha ratiba.

Kaseja ambaye ndiye kipa pekee aliyeiongoza Simba kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2006, alizuia mashuti ya mastraika wa Emmanuel Okwi na John Bocco huku Edward akifunga bao pekee kwenye mchezo huo dakika za mwisho.

Kabla ya kuwakabidhi Simba kombe lao jana, Rais John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi alitema cheche huku akisisitiza kwamba yeye ni shabiki wa Taifa Stars lakini ataisapoti klabu yoyote ambayo itashinda kama Simba ilivyofanya msimu huu.

Simba ilipoteza mechi yake ya kwanza ya ligi, siku chache baada ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ambayo Yanga haina uhakika hata wa nafasi ya pili. Bao pekee la Kagera lilifungwa na Edward Christopher dakika ya 85 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Japhet Makarai.

Simba katika mchezo wa jana walionekana kushambulia lakini walipoteza nafasi nyingi za wazi huku Kagera ikitulia zaidi na ikihamasishwa na Kaseja ambaye aliwajaza upepo wenzake akiwaambia hakuna kupoteza mchezo na hilo lilidhihirika alipopangua penalti ya Okwi dakika za nyongeza.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, kombe hilo linagharimu zaidi ya Sh.10milioni ambazo zinalifanya liwe ghali kuliko lile ambalo Yanga walikuwa wakilitwaa misimu mitatu mfululizo iliyopita. Rais Magufuli alilikabidhi kombe hilo mbele ya umati wa mashabiki wa Simba ambapo uwanja ulikuwa umatapakaa rangi nyekundu.

No comments:

Post a comment