Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ilizindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ili kuhakikisha wakopaji wakiwemo wajasiriamali wadogo wanalindwa na kupata haki zao bila kudhurumiwa wanapo hitaji mikopo na huduma zingine za kifedha zitakazowasaidia kujiendeleza kiuchumi.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge Mhe. Khatibu Said Haji aliyetaka kujua hatua za Serikali kuhusu taasisi za huduma ndogo za kifedha (Microfinance) kuwatoza wananchi riba kubwa wanapochukua mikopo.

Dkt. Kijaji, alisema kuwa  mwezi Desemba, 2017 Serikali ilizindua sera ya huduma ndogo ya fedha itakayosaidia  kuwatambua wakopeshaji  na kuwalinda wakopaji wanaohitaji huduma katika taasisi hizo zikiwemo za mikopo.

“Tunataka kuhakikisha tunawalinda wakopaji na kuhakikisha wanakopa kwa kuzingatia sheria na taasisi hizo za fedha zinazingatia sheria, utaratibu na kanuni za utawala bora”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kukamilika kwa sheria ya huduma ndogo ya fedha hivi karibuni kutakua ni muarobaini wa kutatua changamoto za kifedha kwa wananchi wanaohitaji mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Akijibu swali la Msingi la Mbunge huyo kuhusu hatua za Serikali za kuhakikisha Benki nchini zinapunguza riba ili kuchochea shughuli za biashara, Dkt. Kijaji alisema kuwa Sekta ya Benki inafanya biashara huria na ilianza tangu mwaka 1991 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya Mwaka 1991.

“Kupitia Sheria hiyo, wawekezaji walifungua benki binafsi nchini na gharama za huduma na bidhaa kuamuliwa na nguvu ya soko hivyo Serikali haina mamlaka ya moja kwa moja ya kupunguza viwango vya riba katika soko”, alisisitiza Dkt. Kijaji.

Hata hivyo alizitaja hatua ambazo Serikali imezichukua kwa upande wake kuwa ni pamoja na kuzitaka benki za biashara kutumia Mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji, Benki Kuu kuanza kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89 na pia kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.

Hatua zingine ni Benki Kuu kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa  na Benki za biashara  kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0  na pia Serikali kuendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Aidha Naibu Waziri huyo ameipongeza benki ya CRDB, NMB na Benki ya ABC kwa kupunguza riba ya mikopo kutoka asilimia zaidi ya 20 hadi kufikia asilimia 17 hivyo kuwa na tumaini kuwa Benki zingine zitaendelea kufanya hivyo.

Imetolewa na;
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Share To:

msumbanews

Post A Comment: