Friday, 4 May 2018

Rais Magufuli Kataja Sababu Inayomfanya Asiende Nje ya Nchi Mara Kwa Mara


Rais Dkt. John Magufuli amefunguka sababu inayomfanya asipende kwenda nchi za nje mara kwa mara kwa kudai anahitaji muda wa kutosha kushughulika na matatizo ya wananchi waliomuamini na kumchagua kuwa kiongozi wa nchi.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Mei 04, 2018 wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi barabara ya Kidatu Ifakara mkoani Morogoro yenye urefu wa kilomita 66.9 na kuongeza kuwa viongozi wanaomsaidia ndiyo wanajukumu la kusafiri nje ya nchi na kuhudhuria vikao mbalimbali.

“Kwa sababu mimi ni Rais wa Tanzania, muda wangu mwingi nitatumia kuzunguka kwa wananchi ili nijue shida na vilio vyao, kwa hiyo nazunguka maeneo mengi ya watanzania ili kero zao niweze kuzijibu, na hili ndiyo jukumu langu na ninataka muamini hivyo. Makamu wangu wa Rais atazunguka kweli kwenda nje” amesema Maguful.

Rais Magufuli amesema amepokea mialiko zaidi ya 60 kutoka nchi mbalimbali duniani lakini amekua akiwatuma wasaidizi wake ili kumuwakilisha katika nchi hizo.

Barabara hiyo iliyopo eneo la Nyandeo-Kidatu mkoani Morogoro ina urefu wa kilomita 66.9 itajengwa kwa fedha za serikali, Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (BFID) na itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 104.9.

No comments:

Post a Comment