Friday, 25 May 2018

Prof. Mbarawa azindua maadhimisho ya miaka 50 ya bodi ya Usajili Wahandisi


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa  amezindua maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya usajili ya Wahandisi (ERB) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1968.

Akizindua bodi hiyo jana jijini Dar es Salaam  amesema serikali ikiwa kwa kipindi hiki cha  kujenga uchumi wa viwanda, inakabiliwa na uhaba wa wahandisi wa bandari, posta na reli.

“Niya ya serikali ni kuwa na wahandisi wengi ili kuiwezesha nchi  kufikia ya viwanda, lakini bado kuna baadhi ya maeneo yanachangamoto ambayo ni uhandisi wa bandari,  posta, na reli,” alisema Mbarawa.

Mbarawa alisema mkakati wa serikali kwa sasa ni kuwashirikisha vijana kutoka vyuo vikuu wanaosomea fani ya uhandisi katika kila mradi mkubwa  utakaofanyika hapa nchini waweze kunufaika.


Alisema katika kila mradi utakaotekelezwa nchini ukiwa na kijana kutoka chuo kikuu kutawezesha kuongeza ujuzi wa wataalamu wa uhandisi nchini pamoja na kuongeza idadi yao.

“Kwa mfano kwa sasa tunaliboresha shirika la ndege, lakini tuna uhaba mkubwa wa  wahandisi wa ndege, sasa tukiwajenga vijana mapema, kutaliwezesha taifa kuwa na wahandisi wengi hapo baadaye,” alisema Mbarawa.

Alisema zaidi ya Wahandisi 2,000 wanahitimu masomo katika vyuo vikuu nchini kila mwaka, lakini kati yao ni 800 tu wanaosajiliwa na ERB, hali inayosababisha kuwapo kwa wahandisi wachache nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema alisema idadi ya wahandisi waliosajiliwa nchini ni 21, 742 kati ya hao wahandisi wanawake ni 2,153 sawa na aslimia 10.

Alisema Idadi ya wahandisi wanawake nchini imekuwa ikiongezeka na kwamba mwaka 2010  walikuwa  96 tu  na hadi sasa imefikka 443, hiyo ni kwa jitihada ya nchi ya Norway ambao wamekuwa wakitoa ufadhiri wa masomo.

Prof. Lema alisema licha ya kuwa na idadi hiyo, lakini  idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na mahitaji ya nchi  inavyowahitaji wahandisi katika sekta ya  Ujenzi.

” Juhudi zinapaswa kuongezwa katika udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu, kwa maana idadi ya wanafunzi wa kihandisi wanaodahiliwa katika vyuo vikuu inapungua kila mwaka,” alisema  Lema.

Alisema changamoto inayoikabili taaluma ya uhandisi ni uhaba wa wahandisi, uhaba wa bajeti, uhaba wa rasiliamali watu na fedha, hivyo kama kozi za uhandisi zitaongezwa katika vyuo zitaleta tija baadaye.

No comments:

Post a comment