Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba kulieleza Bunge sababu za wabunge wa Viti Maalum kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo wanayotokea.

Peneza amesema kama kweli Dk Mwigulu anataka kuwa Rais wa Tanzania siku zijazo, akishindwa kulishughulikia jambo hilo atakuwa amepoteza sifa hiyo kutokana na kuzima ndoto za wanawake na vijana.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2018/19  Peneza alisema polisi wamekuwa wakikandamiza demokrasia,  ikiwamo kuwazuia kufanya mikutano kwenye mikoa yao.

“Kaka yangu, Mwigulu kama ulitegemea kuwa Rais siku moja, wabunge wa viti maalum wapo humu kwa mujibu wa Katiba ambayo inazungumzia uwepo wa wabunge wa viti maalum ambao majina yao yanapendekezwa na vyama vyao,” alisema Peneza.

“Lakini mimi pamoja na wabunge wengine tumekuwa tukizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, wabunge tunaambiwa tufanye kazi nyumbani?  Wabunge wa viti maalum tunadhalilishwa, mtuache tufanye kazi.”

Alisema, “Kwa nini tunalipwa fedha, tunahitaji tufanye mikutano kwani tunalipwa, lazima tuwasikilize wananchi na turuhusiwe kufanya mikutano katika maeneo yetu na mwisho tutasema Serikali ya awamu ya tano haitaki wanawake wafanye siasa.”

Alisema kupitia mikutano ya hadhara ndiko ambako wanaibuka wanawake na vijana akiwamo yeye.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: