Ligi ya Wilaya ya Pangani (Aweso Cup) imezinduliwa rasmi Jumamosi hii (April 4 2018) kwa mechi ya mashabiki wa Simba na Yanga iliyokuwa na msisimko mkubwa kutokana na uwepo wa Afisa Habari wa Simba, Haji Manara pamoja na aliyekuwa Afisa Habari wa Yanga, Jerry Murro.




Katika mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Juliana Shonza, ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa goli mbili huku Yanga ikipata goli moja na wekundu hao wa msimbazi kuondoka kitita cha tsh 50000 pamoja na zawadi mbalimbali yakiwemo maziwa Asas.
Baada ya zoezi hilo, timu ishirini za Aweso Cup ambazo zinatarajia kuanza kutimua vimbi Jumapili hii, zilipewa jezi na Mbunge na jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji pamoja na vifaa vingine vya michezo ikiwemo mipira.
Akiongea katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Habari, Juliana Shonza amesema amefurahishwa na hatua ya mbunge huyo kuanzisha ligi hiyo ambayo inakwenda kufungua fursa na kuikomboa wilaya ya Pangani kiuchumi.
“Hongera sana Mhe. Aweso kwa kazi nzuri uliyoifanya kwaajili ya watu wako wa pangani, michezo ni ajira kwa vijana pia inaweza kufungua fursa mpya kwa Wanapangani na kupunguza tatizo la ajira. Kama leo tunaona kuna wasanii wengi wamekuja hapa kwaajili ya Aweso Cup, hawa ni mabalozi wazuri kwaajili ya mji wetu, watatangaza utalii wetu, tunajua hapa kuna mbuga ya Sadani, kwaahiyo hii ni fursa kwa wanapangani na tunajua kupitia michezo kuna vitu vingi vitakuja. Pia nitawaagiza watu wa TFF waje huku kwaajili ya kuboresha mambo mbalimbali pamoja na kutoa ushauri,” alisema Shonza.
Naye Mbunge wa Pangani, Juma Aweso amesema anataka kuifanya Wilaya ya Pangani irudishe heshima yake katika mpira wa miguu.
“Pangani kwa miaka ya nyuma ilikuwa ikifanya vizuri kimichezo lakini kipindi cha kati kuna mambo fulani yalisimama, mimi kama Mbunge na Naibu Waziri wa Maji nikaona ngoja nianze na kuamsha hamasa katika mpira na tukiweza hili kila kitu kitaenda sawa Pangani, barabara yetu ilikuwa changamoto kubwa sana lakini nilipiga kelele bungeni na tayari wametenga bajeti kwaajili ya barabara, mambo ya barabara yakikamilika bila shaka kitu kitakuwa vizuri, uchumi utafunguka upya, kuna mto pangani kwa sasa hivi unaweza kufungua fursa mpya kilimo,” alisema Waziri.
Kwa upande wa kikundi cha wasanii cha Uzalendo Kwanza kinachoongozwa na Steve Nyerere, kiliweza kuhamasisha mchezo huo hali ambayo ilisababisha mchezo huo wa mashabiki wa Simba ya Yanga kuwa na msisimko mkubwa sana.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: