Saturday, 19 May 2018

KAGERA SUGAR: TUTATIBUA SHEREHE ZA SIMBA SC


WAKATI wapenzi na mashabiki wa Simba wakiendelea kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema ataitia doa sherehe hiyo.

Mashabiki wa Simba, hivi sasa wanasherehekea ubingwa wa ligi kuu baada ya timu yao hiyo kutwaa hivi karibuni bila ya kupoteza mchezo katika ligi hiyo ambapo mpaka sasa imeshacheza mechi 28, wameshinda 20 na sare nane, zikiwa zimebaki mechi mbili kukamilisha ligi hiyo.

Simba itapambana na Kagera Sugar, leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo baada ya mchezo huo Simba itakabidhiwa kombe lake la ubingwa wa ligi kuu.

“Niwapongeze Simba kwa mafanikio waliyoyapata msimu huu ukilinganisha na misimu mingine mitano iliyopita lakini wajiandae kukumbana na upinzani mkubwa hiyo Jumamosi.

“Hatutakuwa na cha kupoteza katika mechi hiyo ila kikubwa tunataka heshima, kwa hiyo tutaingia uwanjani kwa ajili ya kutafuta ushindi na siyo kitu kingine ili tuweze kuitia doa rekodi yao hiyo ya kutofungwa mpaka sasa ambayo pia tunaamini itaharibu sherehe zao za kusherehekea ubingwa huo,” alisema Maxime ambaye msimu uliopita alinyakua tuzo ya kocha bora wa ligi kuu.

No comments:

Post a comment