Tuesday, 22 May 2018

Joshua Nassari: Serikali Inawarudisha Watanzania Enzi za Ukoloni

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema) Joshua Nassari amesema Serikali imewarudisha Watanzania katika kipindi cha ukoloni ambako waliporwa ardhi yao bila sababu za msingi.

Nasari amesema kitendo cha kuwachomea nyumba wananchi wa Meru kinawakumbusha miaka ya 1950, ambapo walilazimika kuchanga fedha na kumtuma Japhet Kilila Nguro kwenda Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutetea ardhi yao.

Akichangia katika hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, jana Mei 21, mbunge huyo alizungumza kwa hisia kali kuwa jambo kama hilo linawakumbusha mbali Watanzania na kuona kuwa bado wako katika kipindi cha ukoloni walipokuwa wakiporwa ardhi bila hata kusikilizwa.

“Mimi sijui tunawasaidia akina nani Tanzania yetu hii, wafanyabiashara wanalia, wavuvi wanalia, wananchi wanalia na mnawapora ardhi hivi mnataka kutawala nani lakini?” Alihoji Nasari

Alisema mali walizoachiwa Watanzania na Mungu zimeshindwa kuwa baraka tena na badala yake zimegeuka kuwa laana kwa Watanzania na kuwafarakanisha.

“Mnatutonesha kidonda sisi watu wa Meru, angalia picha hizi zinaonyesha haya ni maganda ya risasi na hizi ni picha za mifugo ambayo imedhoofu sana iliyosababisha wananchi kubaki maskini kabisa,” alisema Nasari

No comments:

Post a comment