Friday, 1 June 2018

Dk Bashiru abadili msimamo Katiba mpya...."Siwezi Kuchambua Tena ,Mnataka Nifukuzwe?"

Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema msimamo wake kuhusu mabadiliko ya Katiba utakuwa tofauti na ule aliokuwa nao awali kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa za CCM kwa kuwa sasa ataendana na maelekezo ya chama hicho.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru alionekana kuwa ni mpigania demokrasia na haki wakati akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akishiriki katika midahalo na mahojiano na vituo vya redio na televisheni kuhusu mijadala ya kitaifa. 

Mwaka 2014  Dk Bashiru alisema Katiba ya sasa “haiwezi kuwa medani ya muafaka wa kitaifa kwa sababu ilisimamia msingi na muafaka wa kitaifa katika chama kimoja”
  

 “Tangu mwaka 1992 wanasiasa wamekuwa wakidai Katiba mpya kwa hoja hiyo; kwamba tuko katika mazingira mapya ya kisiasa, mahitaji mpya ya kisiasa, tuna hatua mpya matarajio mapya, changamoto mpya, taratibu mpya za kuendesha nchi,” alinukuliwa  Dr Bashiru katika mahojiano enzi hizo kabla hajaingia katika siasa za CCM.

Sasa amebadili msimamo,  na msimamo wake utategemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM.

“Leo nazungumza kama katibu mkuu, yaani swali lako lina majibu humo humo,” alisema Dk Bashiru jana alipoongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.

“Ukiwa mchambuzi, unachambua kweli kweli. Ukiwa msemaji wa chama, unawasilisha yaliyoamuliwa kwenye vikao.

“Halmashauri Kuu ndio chombo kikuu kilichoniteua na inaweza kunifukuza. Kwenye uchambuzi kule nisingeweza kufukuzwa.

“Hapa kama wewe unanitakia mema, siwezi kuchambua yale ambayo hayajaamuliwa na vikao. Lakini jambo kubwa nchi hii kama tutaheshimu katiba za vyama vyetu na Katiba za Serikali zetu mbili zilizopo, tunaweza kuanzia hapo kujadili namna ya kurekebisha Katiba hii.

No comments:

Post a Comment