WAKATI serikali ikitangaza kutoa ajira mpya 49,356 katika sekta zake zote mwaka ujao wa fedha, Bunge limeitaka kuajiri walimu wapya 113,359, ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada hiyo uliopo nchini kwa sasa.

Aprili 16, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika, aliliambia Bunge mjini hapa kuwa serikali itatoa ajira kwa idadi hiyo ya wataalamu wakiwamo walimu 16,000 wa shule za msingi na sekondari 16,000 katika mwaka wa fedha 2018/19.

Mkuchika alisema kada ya afya itakuwa na nafasi 15,000 na nafasi zilizobaki zitakuwa ni kwa ajili ya kada zingine zikiwamo kilimo, uvuvi, mifugo, vyombo vya ulinzi, magereza, uhamiaji, watendaji na wanataaluma.

Huku serikali ikipanga kuajiri walimu 16,000, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imesema walimu wapya 113,359 wanatakiwa kuajiriwa, ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika kada hiyo.

Akiwasilisha bungeni mjini hapa jana taarifa ya kamati kuhusu makadirio ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka ujao wa fedha, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, alisema wamebaini kuna uhaba mkubwa wa walimu nchini.

Mbunge huyo wa Nzega Mjini (CCM) alisema kamati ina taarifa kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za msingi nchini ni 273,454 lakini waliopo ni 175,946, hivyo kuwapo upungufu wa walimu 97,508 sawa na asilimia 35.6 ya mahitaji.

Kwa upande wa sekondari, Bashe alisema kamati imebaini mahitaji halisi ni walimu 35,136 lakini waliopo ni 19, 285, hivyo kuwapo upungufu wa walimu 15,851 (asilimia 45.1).

"Serikali haina budi kuchukua hatua za makusudi kuongeza ajira za walimu kunusuru taifa kwani walimu wengi wapo mitaani hawana ajira," alisema Bashe.

Alisema walimu ni nyenzo muhimu katika sekta ya ualimu, lakini waliopo nchini hawatoshelezi mahitaji, hali iliyosababisha kuzorota kwa elimu.

“Pamoja na kuwa suala la ajira ya walimu lipo chini ya Tamisemi (Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), pale kiwango cha elimu kinaposhuka ni wizara hii (ya elimu) ndiyo inayoulizwa na hata kusemwa vibaya,” Bashe alisema.

Aliongeza kuwa kamati yao imebaini Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za kusini mwa Jangwa la Sahara, bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wahadhiri katika vyuo vikuu hususan wenye Shahada ya Uzamivu (PhD).

“Wahadhiri hao wamekuwa wakihama kutoka katika utumishi wa ualimu na kwenda kutekeleza majukumu mengine nchini zikiwamo teuzi mbalimbali ambalo ni jambo jema sana,” alisema na kuongeza:

“Kamati inaishauri serikali kuhakikisha inapata wahadhiri wengine wenye PhD kwa kutenga fedha za kuwapeleka kusoma, ili wakirudi watengeneze wasomi wengine ambao wataendelea kulitetea taifa letu maendeleo.”   

KUHAMISHIWA MSINGI Aliongeza kuwa kamati haiungi mkono uamuzi wa serikali kuwachukua walimu wa shule za sekondari kwenda kufundisha shule za msingi, akieleza kuwa wanaona si sawa kwa kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo na mafunzo yake mahsusi.

“Si hivyo tu, kitendo cha kumchukua mwalimu wa sekondari kwenda kufundisha shule ya msingi kimepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa jamii na walimu wenyewe kuhisi kuadhibiwa, hivyo kushusha morali ya kufanya kazi,” alisema.

BODI YA WALIMUBashe pia alisema kamati yao inaona kuna haja serikali kuunda Bodi ya Taaluma ya Walimu ambayo kama ilivyo kwa bodi zingine, mfano ya makandarasi, itakuwa na jukumu la kufuatilia ubora wa elimu inayotolewa na walimu kwa watoto.

Aliongeza kuwa kamati yao inaishauri serikali kutenga fedha za kutosha kwa Idara ya Ukaguzi, ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi wa shule ambayo wamebaini kwa sasa hayatekelezwi ipasavyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: