Wednesday, 30 May 2018

Aliyemwokoa mtoto Ufaransa atakiwa kurudi Nyumbani


RAIS wa Mali, Ibrahim Boubacar Keïta amemtaka kijana shujaa, mhamiaji kutoka nchini kwake, Mamoudou Gassama aliyemwokoa mtoto mdogo aliyekuwa amening’inia kwenye kibaraza cha ghorofa ya nne katika jengo refu jijini Paris, Ufaransa arudi nyumbani kwani amemwandalia kazi Jeshini.

Balozi wa Mali nchini Ufaransa, Toumani Djimé Diallo akizungumza na kijana huyo katika ofisi za ubalozi wa nchi hiyo na kumpa pongezi kutoka kwa rais wa Mali, maemwambia kuwa Rais anamtaka arudi nyumbani kwao Mali amemwandalia nafasi ya kazi katika Jeshi la nchi hiyo.

Mamoudou alipanda jengo hilo refu bila kutumia vifaa vyovyote huku akishangiliwa na watu waliokuwa wamekusanyika nje ya jengo hilo, hadi kufanikisha kumfikia mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka minne na kumuokoa.

Kitendo hicho cha kishujaa kilichofananishwa na ushujaa uliwahi kuoneshwa na ‘Spiderman’, uliteka mitandao ya kijamii huku video yake ikivuta hisia za wengi waliotaka atunukiwe uraia na maisha bora kwa kujitoa kuokoa maisha.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alimualika kijana huyo Ikulu na kuzungumza naye, kisha akampa cheti maalum cha kutambua ushujaa wake na kuamuru apewe uraia wa Ufaransa baada ya kusikia jinsi alivyohangaika kuingia nchini humo.

Rais Macron amempatia kazi Mamoudou katika Jeshi la Zima moto la Ufaransa, pia amemtunukia medali ya kipekee ya ushujaa kijana huyo na kuwataka raia wote kuiga mfano wake.

No comments:

Post a comment