Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeumizwa vikali na baadhi ya makampuni yanayowatumia vibaya wasanii wa muziki na waigizaji wa filamu kwenye matangazo yao kwa kuingia nao mikataba mibovu ambayo haina faida kwa watu hao.
Picha inayohusiana
Waziri Mwakyembe
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe juzi bungeni wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara yake.
Waziri Mwakyembe amesema amechukizwa na kitendo cha Mzee Majuto kuomba achangiwe fedha kwa ajili ya matibabu ile hali anaonekana karibia nusu ya mabango yote ya matangazo hapa nchini na kutangaza kiama kwa makampuni na taasisi zinazonyonya wasanii.
Kwa kweli dhuluma kwa wasanii ilikuwapo kubwa sana kwa kutumia ‘middle men’ (watu wa kati), watu wenye fedha wamechezea sana wasanii wetu. Hili limeanza kubadilika tumeanza kuwa-empower (kuwawezesha) wasanii wetu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wasitumie middle men,“ameeleza Waziri Mwakyembe.
Kwa mfano vijana wetu wazuri kama kina Kanumba, amefariki kila mtu anajua ni milionea, hapana.. waliotajirika ni wengine. Leo hii mwanasanaa mzuri mzee majuto anaumwa, anaomba fedha, mimi nachanga kutoka mfuko kwangu, maisha yenyewe unayaelewa waheshimiwa.. lakini nusu ya mabango ya biashara ni ya Mzee Majuto.“amesema Mwakyembe.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe tayari ameshateua kamati maalumu ya wanasheria ambayo itapitia upya mikataba yote ya wasanii na waigizaji kwa kuanzia na Makampuni yaliyowahi kufanya kazi na Mzee Majuto na Marehemu Steven Kanumba.
Naomba sasa nitumie nafasi hii kueleza kwamba nimeunda Kamati ya wanasheria, tunaanza na kesi ya Mzee Majuto, Mashirika yote na makampuni yote yaliyoingia mikataba na Mzee Majuto tutaipitia upya mikataba hiyo, kama ameonewa ni lazima ilipwe familia yake, tumeshachoka. Na tukishamaliza tunarudi kwa Kanumba na msanii yeyote ambaye anaona aliingia mkataba wa kipumbavu aje atuone.“amemaliza Waziri Mwakyembe.
Familia ya Mzee Majuto Jumatano Aprili 25, 2018 ilijitokeza kuomba msaada wa hali na mali kwa Watanzania ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: