Leo Jumapili Aprili 15, 2018 Chama cha ACT Wazalendo kimetoa tathmini na uchambuzi wake juu ya ripoti  mpya ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.

Soma taarifa hiyo iliyotolewa leo Aprili 15, 2018 na Kiongozi wa ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, Prof. Mussa Assad ametoa taarifa yake ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka 2016/17. Kwa sasa taarifa hiyo iko wazi kwa umma, baada ya kuwa imekabidhiwa rasmi bungeni. Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali, kama chama cha Upinzani bungeni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu Magufuli tayari amechukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye hati isiyoridhisha, hatua hii ni ya njema, ACT Wazalendo tunampongeza kwa jambo hilo. Hata hivyo, baada ya kuipitia ripoti husika, tumegundua kuwa CAG ameibua masuala mazito ambayo yana madhara makubwa kwenye mfumo mzima wa Bajeti ya Nchi kama hayatashughulikiwa. Tumewaita hapa kuyazungumzia hayo.

Maeneo 8 ya Hatari Katika Ripoti ya CAG.

1. Mawaziri Wanavunja Sheria ya Ukaguzi. Tunaomba kutoa angalizo na muongozo wa kisheria juu ya hadaa inayofanywa na Serikali juu ya kinachoitwa “Majibu ya Mawaziri juu ya Ripoti ya CAG”. Kisheria Mikutano hii ya Mawaziri na wanahabari inayoendelea ni kinyume na Sheria ya Ukaguzi ya Umma, kifungu cha 38(1) na (2), ambacho kinaelekeza waziwazi kuwa Maafisa Masuuli ndio wanapaswa kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na CAG, tena majibu husika hupaswa kuletwa mbele ya Kamati za Bunge za PAC na LAAC. Kwa utaratibu wa kawaida wa kiwizara, maafisa masuuli ni Makatibu Wakuu wa Wizara na si Mawaziri.

2. 6% ya Fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilizokwenda. Katika ukaguzi wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kuwa kati ya Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi 25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4.2 trilioni, sawa na 15% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Jambo la kushtusha na linalohitaji majibu ya Serikali ni kwamba, CAG amegundua kuwa katika fedha zote zilizokusanywa, shilingi 25.3 trilioni, ni shilingi 23.8 trilioni tu ndio zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za serikali na riba, shilingi 1.5 trilioni zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi. Fedha hii ambayo matumizi yake hayajulikani ni sawa na 6% ya Fedha zote zilizokusanywa mwaka huo. Matrilioni haya ambayo Serikali imeyapoteza ni zaidi ya mara mbili ya Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka husika (672 bilioni).

3. Bajeti ya Tanzania haina Hadhi (Credibility) tena. Taarifa ya CAG inaonyesha kuwa Bajeti inayopitishwa na Bunge haina Hadhi (Credibility) tena, kwani kuna matumizi makubwa ya nje ya Bajeti kinyume na ilivyoidhinishwa na Bunge. Kwa mfano, CAG ameonyesha kuwa Bunge lilitoa Kibali kwa Serikali kukopa mikopo ya ndani yenye thamani ya TZS 5.4 trilioni lakini Serikali ilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa kwa 10%, ambapo zilikopwa shilingi 5.9 trilioni, yaani bilioni 500 zaidi ya ukomo wa kukopa uliotolewa na Bunge. Haya ni matusi makubwa kwa Bunge, yanaondoa hadhi ya bajeti inayopotishwa na Bunge.

4. Heshima na Hadhi ya Bunge letu vinaondolewa. Kazi Kuu ya Bunge ni kuidhinisha Bajeti inayoletwa bungeni na Serikali, mara baada ya mjadala. Kwa sasa heshima na hadhi ya Bunge vinaondolewa kutokana na Bajeti iliyopitishwa kutokutekelezwa, hasa kwa kiasi cha fedha zilizoidhinishwa na bunge kwaajili ya miradi ya Maendeleo kutokutolewa. Taarifa ya CAG imeonyesha kuwa, kwa ujumla, ni 68% tu ya Bajeti ya Maendeleo ndio ilitekelezwa, hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Serikali za Mitaa, ambapo ni 51% tu ndiyo ilitekelezwa.

5. Mabilioni ya Fedha za Watanzania yametumika kulipa Madeni ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Taarifa ya CAG imeonyesha pia kuwa Serikali ilitumia zaidi ya shilingi 219 bilioni, kulipa madeni ya nyuma. Lakini matumizi hayo hayakuwa sehemu ya Bajeti iliyoletwa na Serikali na kuidhinishwa na Bunge. Hivyo madeni hayo ni hewa, na ulipwaji wake ni matumizi nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge.

6. TRA Wametoa Takwimu za Uongo za Mapato ya Kodi ya zaidi ya shilingi 2.2 trilioni. Taarifa ya CAG imeonyesha, kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, Mamlaka ya Mapato nchini, TRA ilituhadaa kwa kutangaza kuwa imekusanya fedha zaidi kuliko uhalisia wake. Kati ya kiasi cha shilingi 15.1 trilioni ambazo TRA ilitutangazia kuwa imezikusanya kwa mwaka 2016/17, shilingi 2.2 trilioni hazikuwa za TRA. Kimsingi fedha hizo si makusanyo ya kodi, bali TRA walizikusanya tu kama wakala wa asasi, taasisi na wakala nyengine za Serikali. Makusanyo halisi ya fedha za kodi yalikuwa ni shilingi 12.9 trilioni tu. Uongo huu wa TRA kutangaza hata mapato yasiyo yake umepelekea kutokea kwa shilingi 325 bilioni ambazo zilihesabiwa mara mbili (double accounting) kwenye Hesabu Jumuifu za Taifa, na hivyo kuchafua hesabu za Taifa na kuondoa uhalali wake kitakwimu. Pia taarifa ya CAG imeonyesha kuwa TRA hudanganya makusanyo wanayotangaza kila miezi mitatu.

7. Serikali kwa ujumla imepata Hati Chafu. Taarifa ya CAG ya Ukaguzi wa kwanza wa makusanyo na matumizi ya kibajeti ya Serikali ya awamu ya tano, imeonyesha kuwa, kwa ujumla, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imepata Hati Chafu, kwa kuwa Hesabu Jumuifu za Taifa (consolidated accounts) zimepata Hati ISIYORIDHISHA (Chafu). Sababu za kutolewa Hati hii kwenye taarifa ya CAG ni pamoja na fedha kutumika kinyume na mafungu yaliyopangwa na Serikali yenyewe, kupotea kwa shilingi 1.5 trilioni, TRA kutangaza mapato ambayo si yake kuwa ni yake na hivyo kupelekea ‘double accounting‘ (kuhesabiwa mara mbili kwa fedha) kwenye mapato. Hesabu Jumuifu za Taifa ndio Hazina ya Taifa, kupata Hati Chafu ni hatari sana kwa mustakabali wa Taifa.

8. CAG hajakagua Ununuzi wa Ndege. Licha ya kuwa taarifa hii ya CAG ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo kadhaa ambayo CAG ameyaacha, ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17.

Mapendekezo: Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo hayo 8, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:

1. Tunawaomba Wenyeviti wa Kamati za Bunge za PAC na LAAC kufikisha suala Mawaziri kuzungumza kwenye vyombo vya habari kujibu ripoti ya CAG kwa Spika wa Bunge, ili Spika amjulishe Waziri Mkuu juu uvunjifu huu wa sheria unaofanywa na Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano, wakiwemo Mawaziri wazoefu wa taratibu za kibunge kama Waziri William Lukuvi na Waziri Harrison Mwakyembe. Mawaziri hawa wanafanya ‘spinning’ (hadaa) ili kuficha madudu ambayo CAG ameyaibua. Tunawaasa waache jambo hili, na wafuate sheria.

2. Tunaisihi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kuomba kibali cha kukutana haraka na kuagiza Ukaguzi Maalumu wa shilingi 1.5 trilioni ambazo zimepotea na Serikali ya Awamu ya Tano imeshindwa kuzitolea maelezo kutoka kwenye makusanyo ya mwaka 2016/17. Hii ni mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu kwa Serikali kukusanya fedha, kutozigawa kwenye Wizara, Idara, Wakala na Mikoa, kutoonekana matumizi yake na CAG kushindwa kuzikagua. PAC itimize wajibu wake haraka iwezekavyo. Wakati huu ukaguzi huu unafanyika, kama ilivyofanyika kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waliopata Hati Isiyoridhisha, Rais amsimamishe kazi Katibu Mkuu Hazina na Mlipaji Mkuu wa Serikali, kwa kushindwa kusimamia vema Fedha za Umma na kupelekea Hesabu Jumuifu za Taifa (consolidated accounts ) kupata Hati isiyoridhisha ili kupisha uchunguzi huu.

3. Tunalishauri Bunge litake maelezo ya kina ya Serikali kuhusu kukopa bilioni 500 zaidi ya Serikali yenyewe ilivyoomba na kuidhinishiwa na Bunge. Ni matarajio yetu kuwa Bunge litachukua hatua dhidi ya Serikali kwa kukiuka Sheria ya Bajeti ambayo inakataza kabisa Serikali kukopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge. CAG ameonya katika Taarifa yake kwa kusema yafuatayo kuhusu jambo hili “sehemu kubwa ya mtaji wa mabenki unakuwa umefungwa kwenye fedha walizokopesha serikali kwa muda mfupi na muda mrefu; na matokeo yake, riba ya kukopesha kwa watu binafsi inakuwa kubwa na gharama za maisha zinakuwa juu”. Ukopaji wa namna hii unafanya UCHUMI KUSINYAA kwani unaondoa fedha kwenye mzunguko na kushusha uzalishaji.

4. Tunalishauri Bunge liiwajibishe Serikali kwa kutoheshimu Bajeti ambayo Bunge lilipitisha. Bunge linapaswa kulinda hadhi na heshima yake kwa kuhakikisha fedha za maendeleo linazozipitisha zinapelekwa kama ilivyopangwa. Bunge lisipofanya hivyo litaendelea kudharaulika. Spika wa Bunge asimame imara kulinda Mhimili wa Bunge dhidi ya uvunjifu wa sheria wa Serikali kwenye masuala ya Fedha za Umma, hasa wakati huu ambao CAG ameonyesha Fedha nyingi zimetumika kinyume na utaratibu huku fedha za maendeleo zilipitishwa na Bunge zikiwa hazipelekwi.

5. Ni imani yetu kuwa Bunge litawawajibisha wote waliohusika katika malipo ya madeni ambayo hayakuidhinishwa na Bunge letu. Madeni haya pia yanapaswa kujulikana ni yepi kwani CAG anaonyesha kuwa Wizara ya Ujenzi ndiyo imelipa zaidi madeni ya namna hii ambayo hayakuwa kwenye bajeti. Utaratibu wa namna hii ukiachwa bila kuchukua hatua, utatoa mwanya wa fedha za umma kupotea tu bila maelezo yoyote.

6.TRA kwa makusudi, na kwa lengo la kufanya hadaa walitangaza kiwango kikubwa zaidi cha makusanyo kuliko kiwango ilichopaswa kutangaza kuwa imekusanya. Tunatarajia kuwa Bunge litaitaka TRA iombe radhi Watanzania kwa upotoshaji huo ilioufanya na kutaka wote waliohusika kwenye hadaa hii wawajibike. Pia tunawasihi TRA kuzingatia weledi wa kazi yao kwa kutangaza makusanyo yao tu, na kuacha fedha za taasisi na asasi nyengine kama VETA, TPA, Bodi ya Mikopo nk (ambazo TRA huzikusanya kama Wakala wa taasisi hizo) zitangazwe na wahusika wenyewe.

7. Tunaishari Serikali kurejesha utaratibu wa kupanga matumizi ya kila mwezi ya fedha za umma kwa Hazina, na kuacha utaratibu wa sasa wa Ikulu kupanga matumizi ya kila mwezi. Utaratibu huu wa sasa unamuexpose (unamweka kwenye mazingira hatari) Rais, hasa kutuhumiwa kwa ufisadi na kukiuka sheria iwapo kuna makosa ya upotevu wa fedha kama haya ambayo CAG ameyaibua katika taarifa yake na kupelekea hesabu jumuishi za Serikali kupewa Hati Chafu. Tunashauri pia kuachwa kwa mfumo wa Rais wetu kutamka kugawa Fedha kinyume kabisa na Bajeti iliyopitishwa na Bunge.

8. Ni matarajio yetu kuwa katika ripoti ya mwakani ya CAG, Taifa litapata wasaa wa kuona ukaguzi wa ununuzi wa ndege za shirika la ndege la Taifa, ATCL na ukaguzi wa manunuzi ya kandarasi ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Chato. Ni muhimu sana kwa CAG kuona mambo yanayosemwa na umma na kuchukua hatua za ukaguzi kwani yeye ndiye mlinzi wa fedha za umma.

Hitimisho
ACT Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge tusipotekeleza wajibu wake nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu ya nje ya Bajeti na ya kinyume cha sheria. Ni dhahiri, kwa dalili hizi zilizoonyeshwa na taarifa ya CAG, kuwa Wabunge tusipoisimamia na kuidhibiti Serikali ya awamu ya tano, Nchi itafilisika kutokana na maamuzi ya hovyo, yasiyo ya kibajeti, yanayoenda kinyume na kanuni za kifedha na kiuchumi, na yasiyozingatia sheria za Nchi yetu.

Sisi ACT Wazalendo tutaendelea kuichambua taarifa hii ili kuibua masuala zaidi. Haya tuliyoyaeleza leo ni machache sana, hatujagusia kabisa mapungufu kwenye deni la Taifa, kulinganisha na mambo mengi ambayo CAG ameeleza. Tunawahimiza Wabunge na Wananchi kwa ujumla kusoma taarifa ya CAG kwa ukamilifu. Taarifa ya mwaka huu ina hoja nzito kuliko wakati mwingine wowote ule. Haijawahi kupata kutokea Serikali ya Nchi kulidgarau Bunge letu kama ilivyo kwa kiwango kilichoonyeshwa na taarifa ya mwaka huu ya CAG
Share To:

msumbanews

Post A Comment: