Jana, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Chama cha Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva (Tuma) na Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe walilaani kitendo cha mwanamuziki huyo kumshambulia Shonza wakisema hakuwa sahihi na alitumia lugha mbaya.

Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul alimjibu Shonza katika mahojiano aliyoyafanya na kituo cha Redio cha Times siku tatu zilizopita na mitandao ya kijamii, akilaumu hatua ya Serikali kuzifungia nyimbo 15 mwezi uliopita, zikiwamo mbili za kwake.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Dk Mwakyembe alisema amesikitishwa na matamshi yaliyotolewa na Diamond kuhusu kufungiwa kwa nyimbo hizo.

“Maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo za wasanii kwa kukiuka maadili yalifanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa Shonza ambaye analaumiwa na Diamond,” alisema.

“Diamond atambue kuwa Serikali ina taratibu zake na maamuzi ya naibu waziri ni ya wizara. Kama vikao na wasanii tumefanya vingi sana, lakini Diamond hakuwahi kuhudhuria vikao hivyo, si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao cha peke yake.

Alisisitiza, “Sheria ni ya watu wote bila kujali umaarufu au nafasi ya mtu katika jamii, hivyo msanii Diamond anapaswa kutii sheria na mamlaka zilizowekwa.”
Dk Mwakyembe alisema si busara kwa Diamond kushindana na Serikali na endapo ana ushauri wowote, ni vyema akawasilisha kwa njia sahihi, lakini si kumshambulia naibu waziri kwa dharau na kejeli kama alivyofanya.

“Diamond kwa mafanikio aliyoyapata katika muziki, anatarajiwa kuwa mfano bora kwa wanamuziki wenzake. Napenda kuwakumbusha wasanii wote kwamba sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine,” alisema.

“Pamoja na kuwa na kipaji hicho, wasanii wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia tasnia ya sanaa kama ilivyo kwa tasnia nyingine.”
Kutokana na tukio hilo, TCRA nayo ilieleza kuwa inafuatilia mahojiano yake katika kituo hicho kazi ambayo inafanywa na kamati yake ya maudhui.

Ofisa Mkuu Idara ya Utangazaji TCRA, Andrew Kisaka alisema wamechukua uamuzi huo kwa kuwa mahojiano hayo yamefanyika katika kituo wanachokisimamia.

Alisema Mamlaka hiyo inanaangalia zaidi chombo ambacho imekipa leseni na kwamba, masuala mengine yatashughulikiwa na mamlaka nyingine.
Alisema suala hilo kwa sasa linafanyiwa kazi na kamati ya maudhui na kuahidi kulitolea ufafanuzi siku za hivi karibuni akiwataka wananchi kuwa na subira.

Chombo kingine cha Serikali kilichomshukia Diamond ni Basata ambayo kupitia kwa katibu mtendaji wake, Godfrey Mngereza imesema mwanamuziki huyo amefanya makosa kumjibu naibu waziri na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuitusi Serikali.
Alimtaka mwanamuziki huyo kufuata taratibu katika kulalamikia suala hilo ikiwamo kuandika barua kama alivyoelezwa.
Alisema si lazima msanii aandikiwe barua pale anapokosea kama ambavyo Diamond alitaka kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Katika ukurasa huo, Diamond ameandika kuwa naibu waziri huyo angemwandikia barua kabla ya kumfungia.
Pamoja na kumuunga mkono Diamond katika jitihada za kuikomboa tasnia ya muziki nchini, Chama cha Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva kimemuonya kwa lugha anayoitumia.
Katibu wa chama hicho, Samuel Andrew alisema ingawa matatizo yapo, ni muhimu kufuata taratibu wakati wa kudai ili kuepusha vurugu au kuonekana mkorofi.
Alisema anashukuru wamepata wito wa kukutana na Basata, Jumatatu ijayo katika kikao cha ndani ambacho pia baadhi ya wasanii watakuwapo.
Mwanasheria atoa ufafanuzi
Akizungumzia suala hilo kwa mtazamo wa kisheria, mdau wa sanaa nchini, Onesmo Mpinzile, alisema Sheria namba 23 ya Basata ya mwaka 1984, kifungu cha 3, imempa mamlaka waziri kufungia kazi ya msanii au msanii mwenyewe endapo amekiuka sheria na taratibu.
Alisema kwa upande mwingine, sheria hiyo imeipa mamlaka kamili ya kushtaki na kushtakiwa, hivyo kama Diamond aliona hajatendewa haki alitakiwa afuate utaratibu kupata haki yake.
“Diamond anapaswa kuelewa kwamba majibizano ya maneno hayaondoi uhalisia wa kutakiwa kufuata sheria, huwezi kutumia njia ambayo si sahihi kupata haki kwa kuwa mwenzako hakufuata. Huwezi kupata haki kwa mtindo huo,” alisema.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: