Jumla  ya wagonjwa wa akili 55 waliokuwa wametenda makosa mbalimbali yakiwamo ya jinai wakiwa na ugonjwa wa akili, wameachiwa huru baada ya mahakama kutowatia hatiani.

Hayo yameelezwa jana mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi wakati alipowasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Kamati hiyo ilikuwa nchini ya Uenyekiti wa Najma Murtaza Giga.

Profesa Kabudi ameieleza kamati hiyo kwamba, kifungu cha 219 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20, kinampatia Waziri mwenye dhamana ya masuala ya sheria mamlaka ya kuwaachia huru wagonjwa wa akili waliotenda makosa mbalimbali ya jinai yakiwamo ya mauaji.

“Kutokana na mamlaka hayo ya kisheria, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, nilisaini hati ya kuachiliwa huru wagonjwa 55 wa akili waliotenda makosa mbalimbali ya jinai wakiwa na ugonjwa wa akili na hivyo mahakama kutowatia hatiani,” amebainisha Profesa Kabudi.

Aliongeza kuwa kwa muda mrefu wagonjwa hao walikuwa wakihifadhiwa kwenye Taasisi ya Isanga kusubiri amri ya Waziri.

“Na kutokana na hali ya afya zao za akili kuimarika, iliamua waachiliwe huru, ili waungane na familia zao na kuendelea na matibabu wakiwa nje ya taasisi hiyo,” ameeleza.

Pamoja na kuelezea hilo, Profesa Kabudi pia alianisha mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa na wizara pamoja na taasisi zake katika suala zima la utoaji na usimamiaji wa haki katika kipindi cha bajeti cha 2017/2018.

Baadhi ya mafanikio hayo ni kwa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya daawa ilipata ushindi katika mashauri 82 yaliyokuwa na thamani ya Sh 1,064,581,955,743.

Kwa mujibu wake, ushindi huo umewezesha pamoja na mambo mengine maamuzi ya serikali pamoja na sheria za nchi kutobadilishwa kwa msingi wa kukiuka Katiba.

Mafanikio mengine aliyoyataja ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea na utoaji wa ushauri wa kisheria kwenye mikataba na makubaliano mbalimbali yanayofanywa na Wizara Idara na Taasisi za Serikali.

Katika eneo hilo, hadi kufikia Februari mwaka huu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilifanya uhakiki na kutoa ushauri wa mikataba 691 yenye thamani ya Sh 1,720,026,713,823 na Dola za Marekani 1,0884,472,366, mikataba hiyo ilihusu ununuzi, ukarabati wa majengo, utoaji wa huduma za jamii na ujenzi wa barabara.

Aidha, kwa upande wa mali zilizotaifishwa ni pamoja na kilogramu 24.5 za dhahabu yenye thamani ya Sh 2,012,357,164 na fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya Sh 908,019,979.

Mali nyingine zilizotaifishwa ni pamoja na magari matano ya kifahari aina ya Range Rover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika bandari ya Dare s Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba.

Mali nyingine zilizotaifishwa katika kipindi hicho ni pikipiki, mifugo, mafuta na basi la abiria lililokuwa likitumika kusafirishia meno ya tembo zinazokadiriwa kuwa na thamani ya jumla ya Sh 3,242,787, 915.
  
Credit:Habarileo
Share To:

msumbanews

Post A Comment: