sanduku la kura limeibwa, kurejeshwa
Hali ya sintofahamu imeibuka muda huu katika kituo cha Idrisa kata ya Magomeni baada ya wananchi kudai kuwa kuna mtu ametoroka na sanduku lenye kura.
Wakazi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao kwa kuhofia kukamatwa wameeleza kuwa wana uhakika sanduku hilo limechukuliwa na kurejeshwa.
"Kuna gari ilikuja ikaegeshwa pale jirani kabisa na walipo askari halafu ghafla jamaa mmoja akashuka kuzuga zuga hatimaye akanyakua sanduku na kutokomea nalo," amesema mmoja wa wananchi hao.
Amesema baada ya watu kushikwa na butwaa Polisi waliondoka eneo hilo na baada ya muda mfupi walirejea na mtu huyo akiwa na sanduku.
“Yaani wameenda kuweka kura zao halafu wanajifanya sanduku limerudi huo ni mchezo," amesema mwananchi mweingine.
Hata hivyo msimamizi wa uchaguzi wa kituo hicho, Zuhura Mohamed amekanusha kutokea kwa tukio hilo.
"Hakuna kitu kama hicho , mambo yamekwenda vizuri, vituo vilifunguliwa kwa wakati na watu wameonyesha kujitokeza ingawa kasi yao si kubwa sana. Tunaamini wataongezeka,” amesema.
Naye msimamizi wa uchaguzi kituo cha Kwamkunduge kata ya Tandale, Alex Cassian amesema idadi ya wapigakura iliyopo kwenye vitabu vya kupiga kura haiendani na mwitikio wa wapiga kura waliojiandikisha kwenye eneo hilo.
Cassian amesema hadi saa 5:15 asubuhi wapiga kura waliojitokeza walikuwa 60 wakati waliojiandikisha ni 445.
"Hadi muda huu waliopiga kura ni 60 kati ya 445 waliojiandikisha na siku imeisha maana tupo hapa tangu saa 1 asubuhi na nusu siku imeisha kwa kuwa ikifika saa 10 jioni ndiyo mwisho wa kupiga kura," alisema Cassian.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: