Siha. Mawakala zaidi ya 70 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamezuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Siha kutokana na kukosa barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 17,2018 naibu mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa CUF Taifa, Masoud Omar amesema mawakala wao 73 kati ya 75 wamezuiwa kuingia vituoni kutokana na dosari hiyo.

Omar ambaye pia ni meneja wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Siha kwa tiketi ya chama hicho, Tumsifuel Mwanri, amesema wanawasiliana na CUF makao makuu kutatua tatizo hilo.

Amesema ni mawakala wawili tu walioruhusiwa.

Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Valerian Juwal bado hajapatikana kuzungumzia suala hilo.

Awali, mkurugenzi huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa upigaji kura ulioanza saa moja asubuhi ulikuwa ukiendelea vizuri na vituo vyote vilikuwa shwari na kulikuwa hakuna tatizo lolote.

Hali ya ulinzi imeimarishwa kukiwa na  magari yaliyowabeba askari, huku wengine wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakionekana maeneo kadhaa ya jimbo hilo
Share To:

msumbanews

Post A Comment: