Jalada la kesi inayomkabili Mhasibu Mkuu wa TAKUKURU, Godfrey Gugai anayedaiwa kumiliki mali zenye thamani ya Sh. Bilioni 3 ambazo haziendani na kipato chake limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati shauri hilo lilipokuja kwaajili ya kutajwa.

Wankyo alieleza awali  jalada hilo lilipelekwa kwa DPP ambapo alilipitia na kulirejesha TAKUKURU na kuelekeza baadhi ya maeneo yafanyiwe uchunguzi zaidi.

Alidai kuwa maeneo hayo yamekwisha fanyiwa kazi na jalada limerejeshwa tena kwa DPP kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.

Wankyo baada ya kuyaeleza hayo aliiomba Mahakama iipangie kesi hiyo tarehe nyingine ili waweze kueleza hali ya upelelezi ikoje.

Kwa upande wa mshtakiwa Gugai alidai kuwa sasa wamefikisha siku 90 hivyo anaomba kesi ipangiwe siku saba ili waweze kujua hali ya upelelezi ikoje.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi February 21,2018 na kuutaka upande wa mashtaka uhakikishe wanalifanyia kazi jalada hilo kwa kuwa limeanza kuzeeka.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera. Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: