Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe alipokutana nao kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya kisarawe pamoja na kuwashukuru kwa kuchaguliwa katika uchaguzi uliomalizika.
Na Alex Sonna, Kisarawe
Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amewaambia Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuwa kipindi cha miaka mitano ijayo kitakuwa cha mchakamchaka wa maendeleo, akisisitiza kuwa wana jukumu kubwa la kuwatumikia wananchi kwa ufanisi na mshikamano.
Akizungumza katika kikao cha kuwashukuru na kuomba ushirikiano wa madiwani hao, Dkt. Jafo amesema amejipanga kuhakikisha anatafuta rasilimali fedha zitakazosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata zote za wilaya hiyo.
Amesema matarajio ya wananchi ni makubwa, hivyo madiwani wanapaswa kutambua uzito wa dhamana waliyopewa na wananchi.
“Chaguzi zote zimekwisha. Tulianza na kura za maoni, tukapita kwenye uchaguzi mkuu na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri. Kila uchaguzi huwa na makundi, lakini sasa ni wakati wa kuungana na kushirikiana kwa ajenda moja ya maendeleo,” amesema Dkt. Jafo.
Mbunge huyo ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Baraza la Madiwani ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akibainisha kuwa tayari ameshawasilisha maombi mbalimbali serikalini yanayohusu ujenzi wa shule mpya na kuboresha miundombinu ya shule zilizopo.
“Nitahangaika kwa kila hali kuhakikisha tunasonga mbele kama halmashauri. Maombi ya ujenzi wa shule mpya na miundombinu ya elimu yameshapokelewa na serikali,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha sasa atakuwa karibu zaidi na wananchi kwa kufanya ziara nyingi vijijini, kutoa taarifa na kusikiliza changamoto zao, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano.
“Tusikubali kugawanywa, kwa sababu tukiruhusu hilo tutaleta udhaifu. Tufanye kazi kama timu, tushirikiane na tupendane, wote tuwe kitu kimoja,” amesema.
Kwa upande wa sekta ya afya, Dkt. Jafo amesema amejipanga kuweka historia mpya kwa kuhakikisha kila kijiji katika Wilaya ya Kisarawe kinakuwa na zahanati, ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, amewataka madiwani kusimamia kwa karibu matumizi ya mapato ya ndani ili yatumike kwa usahihi na kuleta matokeo yanayo onekana.
“Haiwezekani mwaka ukapita bila kuwa na kitu kinacho onekana kimefanyika. Lazima fedha tunazo kusanya ziwe na matunda kwa wananchi,” amesema.
“Nikuhakikishie Mwenyekiti, miradi ya maendeleo tutahangaika nayo kwa ujumla wake. Tunaahidi mengi vijijini, hivyo ushirikiano na kupendana ni jambo la msingi ili tufanikiwe,” amesema.
Amewahimiza madiwani hao kwenda kuwashukuru wananchi waliowaamini na kuwachagua, akisisitiza kuwa mafanikio ya safari ya miaka mitano ijayo yatategemea namna watakavyoanza na kuendeleza kazi ya kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu.
























