Julieth Ngarabali,   Kibaha. 


Sheik Mkuu wa Mkoa wa Pwani Sheik Hamisi  Mtupa amewahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi iliyo bora na yenye kumcha Mungu ili waklkua baade wawe wazalendo wa Taifa kwenye nyanja mbalimbali.


Sheik Mtupa ambaye ni mwenyikiti mweza wa kamati ya Amani Mkoani Pwani amesema    mfumo wa malezi na makuzi ya awali kwa watoto kuanzia umri wa sifuri (akiwa tumboni ) mpaka miaka minane bado  wazazi na walezi wengi wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa ama ubize au kwa kutoona umuhimu tu hivyo kundi hilo kukua bila ya kuwa na misingi bora ya malezi ambayo ni nguzo kuu ya uzalendo.


"Unajua mzazi anaposhika ujauzito tu hapo tayari anatakiwa aanze malezi , anaweza kuzungumza kitu chochote na mwanaye tumboni na mtoto huyo anakua anamuelewa hii kitu tuamini tusiamini lakini ndivyo ilivyo "amesema Sheik  Mtupa.


Naye Paroko wa Kanisa Katoliki Tumbi Kibaha  Benno Kikudo amesema  jamii inayotoa malezi stahiki na yenye kumcha Mungu kwa watoto sio rahisi wajiingize kwenye makundi ya uvutaji bangi, uvaaji hereni (wavulana) na uporaji mitaani kwa sababu ya msingi wa malezi bora waliyopata toka wadogo.


"Hili kundi ni muhimu sana sisi wazazi na walezi tusisubiri wafikishe miaka  mitatu ama 10  ndio tuzungumze nao apana , tunakosea tutakua tumechelewa mno ,tuanze malezi mapema kama wataalamu wetu wanavyotushauri"amesema Paroko Kikudo


Mmoja wa wazazi mjini Kibaha Alvina Martin amesema kwa kawaida imezoeleka   mawasiliano ya kuzungumza kati ya mama na mtoto hufanyika pale anapozaliwa lakini kupitia mafundisho ya viongozi hao wa dini  sasa wameshapata uelewa kuwa inaanzia umri wa sifuri na kuendelea.


" Niliwahi kumuona mzungu kwenye TV anashika shika tumbo lake huku akimwambia mtoto wewe ni mzuri sana lala muache mama yako afue , niliona kama igizo kumbe ni kitu ambacho napaswa kumfanyia mwanangu hata akiwa tumboni"amesema  Alvina


Mwalimu wa shule ya awali Vigwaza Victor Urio amesema katika malezi na makuzi ya awali shuleni ushirikiano kwa wazazi na walimu ni muhimu zaidi kwa sababu elimu ya awali ni hatua ya kwanza ndani ya mfumo wa elimu ya msingi  ambayo itawezesha kutoa wataalamu watakaolitumikia Taifa.


Awali Mkurugenzi wa shirika la Children in Crossfire (CIC) Crain Ferla linaloshiriki katika programu jumuishi ya Taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (  PJT - MMMAM ) amebainisha programu ya mtoto kwanza wanayoitekeleza hapa nchini  itakua na malengo ya kuinua maendeleo ya watoto ili kuhakikisha kila mmoja anakua katika misingi bora.


Share To:

Post A Comment: