Diwani wa Kata ya Magila- Gereza katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mwajuma Kitumpa (wa tatu kushoto) akiwa na ndoo yenye maji kichwani, mara baada ya kukabidhiwa mradi wa Kisima cha Maji Shule ya Msingi Gereza na Taasisi ya Kidini ya DirectAid Society ya jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa). 

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Gereza, Kata ya Magila- Gereza katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakiwa tayari  kukabidhiwa mradi wa Kisima cha Maji shuleni hapo, na Taasisi ya Kidini ya DirectAid Society ya jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Magila- Gereza  katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Shaaban Kitumpa (kulia) akimtwisha  ndoo yenye maji kichwani mmoja wa wanawake wa kijiji hicho. Ni baada ya hafla ya kukabidhiwa mradi wa Kisima cha Maji Shule ya Msingi Gereza na Taasisi ya Kidini ya DirectAid Society ya jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kidini ya DirectAid Society mkoani Tanga Mohamed Mohamed (kulia) akifungua koki ya maji kwenye hafla ya ufunguzi wa Mradi wa Maji Shule ya Msingi Gereza. Kushoto ni   Diwani wa Kata ya Magila- Gereza katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mwajuma Kitumpa. (Picha na Yusuph Mussa). 

Diwani wa Kata ya Magila- Gereza katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mwajuma Kitumpa (kushoto) akishuhudia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gereza Rehema Kiondo akifungua koki ya maji. Ni baada ya kukabidhiwa mradi wa Kisima cha Maji Shule ya Msingi Gereza na Taasisi ya Kidini ya DirectAid Society ya jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa).

 Na Yusuph Mussa, Korogwe



WALIMU, wazazi, wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Magila- Gereza pamoja na vitongoji vyake, wanatoa shukrani kwa Shirika la Kidini la DirectAid Society kwa kuweza kuwapatia mradi mkubwa wa maji utakaoweza kusaidia zaidi ya wanafunzi  656 pamoja na  wanafunzi wenye mahitaji maalumu 52  jumla yao wakiwa 708 katika Shule ya Msingi Gereza,  na wakazi waishio karibu na shule hiyo wapatao 5,040.


Hayo yalisemwa Machi 2, 2022 na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gereza, iliyopo Kata ya Magila- Gereza, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Rehema Kiondo. Ni kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa kisima hicho kilichojengwa shuleni hapo kwa gharama ya sh. milioni 10.


"Jambo hili ni kubwa sana kwani ni muda mrefu wanafunzi walikuwa wakisumbuka kubeba ndoo na vidumu vya maji kila siku kwa ajili ya usafi wa majengo ya shule, kupikia uji pamoja na usafi wa vyoo. Vile vile  tunamshukuru diwani wetu (Diwani wa Kata ya Magila- Gereza, Mwajuma Kitumpa) kwa usimamizi na uhamasishaji wa jamii na usimamizi makini tangu katika mchakato mzima wa upatikanaji wa mradi huu.


"Kisima hiki kitasaidia kwa kuondoa usumbufu huo kwa wanafunzi, kwani maji haya yatakuwa yanapatikana muda wote. Tunaahidi kutunza mradi huu na vifaa vyote mlivyotupatia ili viweze kutumika kwa muda mrefu. Hatuna maneno mazuri  ya kuzungumza zaidi ya kuwashukuru na kuwaombea Mwenyezi Mungu awazidishie  pale mlipopunguza basi apajaze zaidi na zaidi" alisema Kiondo.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Magila- Gereza Shaaban Kitumpa alisema mradi huo ni mkombozi kwa watoto wa shule hiyo sababu hawatahangaika tena na vigaloni. Lakini pia wananchi wa kijiji hicho watanufaika kwa mradi huo kuletwa kijijini hapo.


"Kuna wenzetu wana shida kama hii, lakin tumepata sisi. Hivyo tuenzi mradi huu ambao ni mkombozi kwa watoto wetu na jamii. Miundombinu tuilinde kwa nguvu zote" alisema Kitumpa.

Diwani wa Kata ya Magila- Gereza Mwajuma Kitumpa aliwashukuru wafadhili hao kwa mradi huo, na anaomba wafadhili hao kujenga mradi kama huo kwenye vijiji vya Mgobe, Kalekwa na Kitongoji cha Kiloza, kwani kitongoji hicho mahitaji yake ya maji ni makubwa kutokana na kuwepo kwa gulio siku ya Ijumaa, na gulio dogo Jumanne, huku idadi ya watu ikiwa kubwa.


Kitumpa pia aliomba wafadhili hao kuwaongezea nguvu ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Magila- Gereza, kwani hadi sasa imegharimu sh. milioni 25 kwa nguvu za wananchi wakisaidiwa na Mfuko wa Jimbo ambao umetoa sh. milioni mbili kwa ajili ya saruji na mabati 120 yaliyoezeka zahanati hiyo, huku wafadhili wenye hoteli kubwa kwenye kata hiyo Kilimanjaro na Rock hill, wakisaidiana na wananchi kufikia hatua hiyo.


"Tukiweza kupata sh. milioni 50, tutaweza kukamilisha zahanati hii ambayo itakuwa pia ni tegemeo hata kwa vitongoji vilivyopo kata za jirani za Mswaha- Darajani na Lutindi na Lewa. Eneo hili lipo barabara kuu ya Arusha- Dar es Salaam, hivyo kukiwa na huduma nzuri kutasaidia watu wanaopata ajali kama ilivyotokea hivi karibuni" alisema Diwani Kitumpa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Miradi ya Shirika hilo Mkoa wa Tanga ambalo Makao Makuu yake yapo Dar es Salaam, na mfadhili wake yupo nchini Qatar, Mohamed Mohamed, alisema miradi wanayotekeleza kwa sasa ni ya mwaka 2021, hivyo katika miradi ya mwaka 2022, wanaweza kuongeza visima vingine kwa kata hiyo ya Magila- Gereza.


"Mpaka sasa kwa Mkoa wa Tanga tumetumia sh. milioni 180 kwa ajili ya uchimbaji wa visima. Kwenye Wilaya ya Korogwe tumechimba visima vinane vyenye thamani ya sh. milioni 80, ambapo kila kisima kimoja kimegharimu sh. milioni 10. Visima hivyo ni Mtonga, Bagamoyo, Kwakombo, Mandela, Segera- Mashine, Old- Korogwe, Kwasunga, na Magila- Gereza.


"Tutazunguka kuona wenye mahitaji zaidi. Kata ya Magila- Gereza ina vijiji vingi havina maji. Tuna uwezo wa kusaidia visima vingine kwa mwaka 2022 baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. DirectAid Society ni mdau wa Serikali, hivyo tupo kuona huduma za maji na mahitaji mengine yanaifikia jamii" alisema Mohamed ambaye ni raia kutoka Misri.


MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: