NAIBU Waziri wa Maji,Maryprisca Mahundi  ameitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa)mkoa wa Simiyu kuhakikisha miradi yote ya Maji inayotekelezwa kupitia fedha zilizotolewa na serikali ikiwa ni Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 inakamilka kufikia mwishoni mwa mwezi April mwaka huu.


Naibu Waziri,Mahundi amesema hayo  wilayani Busega mkoani Simiyu alipotembelea ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye mita za ujazo 50 kwenye mnara wa mita 15  katika kijiji cha Badugu.


Amesema hakuna sababu ya Mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa muda huo kwani fedha kwa ajili ya miradi hiyo ipo kinachotakiwa ni kufanya kazi kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu na kufuata taratibu za kuomba pesa na wao wizara ya maji  hawana urasmu wowote juu ya utoaji wa fedha za miradi ya UVIKO-19 .


Naibu Waziri,Mahundi amemtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo Kampuni ya Jonta Investiment ya Mjini Shinyanga kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika kwa muda uliopangwa.


Awali Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Busega,Mhandisi Daniel Gagala  akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mradi huo amesema  kiasi cha Sh 317,923,663 zitatumika hadi utakapokamilika. 


Amesema hadi sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki,Ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji,Ujenzi wa nyumba ya mambo na ununuzi wa bomba.


Rais Samia Suluhu alielekeza Sh  Bilioni 139.4 za fedha za Uviko 19 kwa Wizara ya Maji kwa lengo la kuhakikisha zinatumika kuondoa changamoto ya maji nchi nzima.


Serikali ya Tanzania ilipokea Sh trilioni 1.3 kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa mapambano ya ugonjwa wa Covid 19.

Share To:

Post A Comment: