Watu wawili wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Katavi kwa tuhuma za mauaji ya Mariam Paschal (36) na mtoto wake Editha Dutu mwenye umri wa miezi minee, kisha miili yao kuifukia katika pori la Kalilankulunkulu lililopo wilaya ya Tanganyika mkoani humo.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Katavi ACP Ali Makame Hamad amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Dutu Maige (30) ambaye ni mzazi mwenza wa marehemu na Yussufu Sita (32). 


Aidha ACP Hamad amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia kati ya mtuhumiwa Dutu Maige na marehemu Mariam Paschal ambaye ni mzazi mwenzake, walikuwa wakigombea mali ambayo ni magunia 60 ya mpunga hivyo mara kwa mara walikuwa wakishtakiana katika ofisi za serikali ya kijiji.


ACP Hamad amesema jeshi la polisi lilipokea taarifa Machi 8 mwaka huu kutoka kwa Paschal Masheku (56) mkazi wa Kijiji cha Sentamaria ambaye ni baba wa marehemu kuwa binti yake huyo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu mwezi Julai, 2021 akiwa na mtoto wake ndipo jeshi likaanza upelelezi wa kina ambapo Machi 9, 2022 walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao  kuhusiana na tukio hilo.


Kamanda amesema awali miili ya marehemu hao ilikutwa kwenye pori hilo ikiwa imeharibika kwa kushambuliwa na fisi na baadae ilifanyiwa uchunguzi na madaktari wa magereza kwa kushirikiana na polisi na kuzikwa.


Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida watuhumiwa hawakuishia hapo baada ya mazishi yaliyofanywa na polisi, watuhumiwa walirudi na kufukua miili hiyo kisha kuipeleka sehemu nyingine na kuichoma moto ilikupoteza ushahidi ambapo baada ya kuwakamata walikiri kufanya mauaji hayo na kuliongoza  jeshi  la polisi walikochoma miili hiyo na kufukia na baada ya kufukua walikuta mabaki ya  mifupa ya mbavu.


Kamanda amesema  baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: