Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Jumbe Wilayani Manyoni jana.

Wazee kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Singida waliotimiza miaka 60 wakikata keki kama ishara ya kusherehekea Miaka 60 ya Uhuru.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.

Mkuu wa Mkoa wa Singida wapili kutoka kulia, akiwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa alhaj Juma kilimba wa kwanza kulia wakiwa na Viongozi wengine akitembelea mabanda katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.
Shughuli ya kutembelea mabanda ikiendelea.
Wafanyakazi kutoka Shirika la Nyumba Mkoa wa Singida wakiwa kwenye banda lao wakimngoja Mkuu wa Mkoa kuja kutembelea.


Na Boniphace Jilili, Singida.


MKOA wa Singida ni miongoni mwa mikoa iliyotoa mchango mkubwa katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kutokana na wananchi wake kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono jitihada za kudai uhuru zikiongonzwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mkuu wa Mkoa huo Dkt.Binilith Mahenge alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara na miaka 59 ya muungano yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Jumbe Wilayani Manyoni.

Alisema mkoa huo ulikuwa na Viongozi mashujaa walioshiriki kikamilifu katika mapambano ya kuwaondoa wakoloni akiwemo Mama Liti Hema aliyewathibiti Wakoloni wa Kijerumani kuingia Singida kwa kutumia makundi ya nyuki ambayo yaliwashambulia na kuwarudisha nyuma Askari hao.

"Kwa taarifa zilizopo hao Nyuki walikuwa wanawashambulia wazungu pekee na sio waafrika,kwahiyo Mkoa wa Singida umechangia nchi yetu kupata uhuru." alisema Dkt.Mahenge.

Dkt.Mahenge alifafanua kuwa kabla ya uhuru Mkoa huo ulikuwa ni moja ya eneo la Utawala wa Mkoloni katika Jimbo la kati (Central Province) na Wilaya ya Manyoni iliteuliwa kama eneo la majaribio na kipimo cha uwezo wa kujitawala ambapo mwaka 1958 aliteuliwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza kabla ya uhuru aliyeitwa Dustan Omary.

Alisema Baada ya uongozi huo wa majaribio wa wazawa kudumu na kutekeleza vema masuala ya Utawala ilileta chachu kubwa ya kudai Uhuru ambao ulikuja kupatikana Desemba 09 mwaka 1961 na baadaye kuanzishwa rasmi mkoa huo Oktoba 15 mwaka 1963.

Dkt.Mahenge alisema tangu kuanzishwa kwa mkoa huo hadi sasa kuna mafanikio mengi ambayo mkoa unajivunia ikiwa ni pamoja na kuongezeka tija katika sekta mbalimbali zikiwemo Uzalishaji mali na huduma za kijamii,Utawala bora pamoja na Ulinzi na Usalama kwa ujumla.

Aidha aliwasisitiza wananchi kutumia fursa nyingi za uwekezaji zilizopo mkoani hapa ambazo wakizitumia vizuri itasaidia kuondoa umaskini wa kipato na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa mkoa huo, kiuchumi na kijamii.

"Kwa miaka sitini ijayo tuongeze nguvu katika kufanya kazi kwa bidii, tutumie kikamilifu rasilimali tulizonazo kwa kuzalisha zaidi bidhaa zilizoongezwa thamani na kutumia fursa za masoko zilizopo." alisema Dkt. Mahenge.

Awali Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Singida Yohana Msitta kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM mkoa aliwaomba waalimu kutoa Elimu kwa vijana ili watambue historia ya nchi ilikotoka kwani maadhimisho hayo ni historia.

"Hawa vijana waliozaliwa baada ya uhuru ni rahisi sana kusahau tulikotoka,hivyo ni vema waalimu nyie hasa mnao kwenda kustaafu mnaifahamu vizuri historia wafundisheni vijana wetu." alisema Msitta.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba Viongozi wa Serikali kusimamia mifumko ya bei za bidhaa mbalimbali ili wananchi waendelee kuwa huru kama ilivyo tafsiri ya uhuru.

Mkoa wa Singida uliungana na watanzania wote katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru kuanzia Desemba 04 hadi 08 Desemba mwaka huu na kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Miaka 60 Uhuru: Tanzania Imara,Kazi Iendelee."  ambapo kilele chake kitaifa kitafanyika Desemba 09 mwaka huu jijini Dar es Salaam.  

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: