Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe ameitaka sekta binafsi nchini kushiriki ipasavyo katika utekelezaji Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 ili kufanikisha jitihada za serikali za kujenga uchumi jumuishi ili kuchochea uchumi na kukuza ajira na kipato kwa wananchi.


Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wenye lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kutoa hamasa kwa sekta hiyo kushiriki ipasavyo katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.


Waziri Mwambe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajiri ya kukabiliana na athari za Uviko -19 ambapo fedha hizo zimelenga kuleta ustawi katika sekta mbalimbali za huduma ikiwemo elimu, afya, maji na utalii.


“Naomba nitumie fursa hii, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake kubwa aliyoionesha katika mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa kuwezesha upatikanaji wa Shilingi Trilioni 1.3 ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ili kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19”, Amesema Mwambe


Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 ulizinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 10 Oktoba, 2021 Jijini Dodoma, Ambapo shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na  Shirika la Fedha Duniani (IMF) zimelenga kuleta ustawishaji katika sekta za huduma ikiwemo Elimu, Afya, Maji na Utalii.*

Share To:

Post A Comment: