Na Tito Mselem, Morogoro


Imeelezwa kuwa Sensa  inayotarajiwa kufanyika Mwaka 2022, itahusisha  kipengele maalum kitakachokuwa na maswali yatakayo kuwa  yakikusanya takwimu za wachimbaji ili kujua idadi yao,  mahali walipo  na mchango wao kwenye pato la taifa. 


Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alipofanya ziara katika Migodi ya Epanko inayochimba madini ya Spinel iliyopo Mahenge wilayani Ulanga mkoa wa Morogoro ambapo amewataka wachimbaji wote wajitokeze kuhesabiwa ili serikali iweze kupanga mipango ya maendeleo katika Sekta ya Madini.


Prof. Msanjila amesema, kujitokeza kwao kutaiwezesha serikali kujipanga vizuri katika  kuendeleza na kuboresha miundombinu katika maeneo ya uchimbaji wa madini.


"Akihesabiwa mchimbaji mmoja, serikali itajua anawatoto wangapi hivyo itasadia serikali  kujua Sekta ya Madini inalea watu wangapi," amesema Prof. Msanjila.


Aidha, Prof. Msanjila amewasisitiza wachimbaji wa madini nchini kuchanja chanjo ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa UVICO-19 ambapo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amejiridhisha kwamba chanjo ya ugonjwa huo ni salama na kuwataka wajitokeze kuchonja. 


Pia, Prof. Msanjila amesisitiza suala la Usalama mahala pa kazi, ambapo amemtaka Afisa Migodi Mkazi wa Wilaya ya Ulanga Robert Erick kuhakikisha anafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika migodi ya Epanko na kuwashauri wachimbaji kabla majanga hayajatokea ili kulinda afya zao.


Kufuatia  hatua hiyo, Prof. Msanjila amesema, ili Wizara ya Madini ifanikiwe, lazima wachimbaji wa madini wafanikiwe ambapo amewashauri wachimbaji hao kujiunga kwenye vikundi na kushirikiana ili waliite Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuchoronga na kubainisha uelekeo wa mashapo ili kuepuka kuchimba kwa kubahatisha.


Akijibu hoja ya Mbunge wa Jimbo la Ulanga Salim Hasham, Prof. Msanjila amesema wilaya ya Ulanga inatarajia kupata uwekezaji mkubwa na wa kati katika uchimbaji wa madini ya _Graphite_ na kuahidi kushirikiana na Wizara ya Nishati ili isaidie kusogeza nishati ya umeme katika maeneo ya migodi ili kupunguza gharama za uzalishaji.


Vile vile, Prof. Msanjila amesema sehemu zote zenye milipuko ya madini wilayani humo lazima zirasimishwe haraka na kutolewa leseni katika maeneo hayo ili kuepuka migogoro isiyo kuwa ya lazima.


Pia, Prof. Msanjila amemtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro  Emmanuel Shija kushirikiana na Afisa Migodi Mkazi wa wilaya ya Ulanga Robert Erick kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini ya Spinel juu ya kutunza kumbukumbu za biashara ya madini na kuwaunganisha na mabenki ili wapatiwe mikopo kwa lengo la kuimarisha shughuli za uchimbaji. 

     

Naye, Mbunge wa Jimbo la Ulanga Salim Maudin Hasham amempongeza Prof. Msanjila baada ya kufanya ziara wilayani humo na kushuhudia mafanikio na changamoto zinazowakabili ambapo alimuomba Prof. Msanjila kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme na barabara bora kutoka Mahenge mpaka sehemu ya migodi.

Share To:

Post A Comment: